Mkuu
wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini Anna Rose Nyamubi (katikati aliyeshika
kipaza sauti) pamoja na Mbunge wa Jimbo la Solwa Salum Ahmed ( wa tatu
kutoka kulia) pamoja na wakazi wa Lyabusalu wilayani Shinyanga Vijijini
wakiimba na kucheza kwenye uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini
uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo wakati wa utoaji wa hotuba ya uzinduzi wa mradi huo
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi huo
……………………………………………………………………………………
Na Greyson Mwase
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini Anna Rose Nyamubi amesema
kuwa kupatikana kwa nishati ya umeme katika wilaya hiyo kutapunguza
mauaji ya vikongwe ambao wamekuwa wakiuwawa kutokana na kuwa na macho
mekundu yanayosababishwa na moshi wa majiko ya kuni.
Nyamubi ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa mradi wa umeme
vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vjjijini (REA) Awamu ya Pili
uliofanyika katika Kata ya Lyabusalu wilayani Shinyanga Vijijini. Mradi
huo ulizinduliwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo
Alisema kuwa katika wilaya ya Shinyanga Vijijini kumekuwa
kukijitokeza mauaji ya wazee wenye macho mekundu kwa dhana ya kuhusishwa
na vitendo vya kishirikina, dhana ambayo ni potofu kabisa
Alieleza kuwa vikongwe wengi wameathirika na moshi wa majiko ya
kuni, yanayopelekea macho mekundu na kuongeza kuwa mara baada ya wilaya
hiyo kupata neema ya umeme na wananchi wake kuanza kutumia nishati ya
umeme kwa kupikia itapunguza waathirika wa moshi wa majiko ya kuni na
kupunguza vifo.
Aliendelea kusema kuwa nishati ya umeme itawezesha wananchi wa
wilaya hiyo kuanzisha viwanda vidogo vidogo kama vya kukoboa nafaka kama
mahindi, mpunga na kujiingizia kipato na hivyo kupunguza umasikini.
“ Wito wangu ni kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hii ya kuwa
na umeme kwa kujikwamua kiuchumi na kubuni miradi mbalimbali badala ya
kutegemea kufanyiwa kila kitu na Serikali.
Mbali na kuwataka wananchi kuunganisha nyumba zao na miundombinu
ya umeme iliyowekwa, amewataka wananchi kuanzisha vikundi vidogo na
kuanzisha miradi midogo itakayowakwamua kiuchumi.
Wakati huo huo akizungumza wakati wa uzinduzi huo Meneja wa
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)- Kanda ya Ziwa, Mhandisi Joyce
Ngahyoma aliwataka wananchi kuchangamkia mradi huu kwa kuunganisha umeme
kwa gharama ya shilingi 27,000 ambayo ni kodi tu kwani gharama zote
zimebebwa na serikali, kabla ya mradi huo kumalizika mwishoni mwa mwezi
Juni mwaka huu.
Mhandisi Ngahyoma alieleza kuwa mara baada ya kukamilika kwa
awamu ya pili ya Mradi wa REA wateja watakaoomba kuunganishiwa umeme
watalipa shilingi 177,000 au kusubiri awamu ya tatu ya mradi wa REA
inayotarajiwa kuanza mapema mwezi Julai.
Akizungumzia suala la uwekaji wa mifumo ya umeme kwenye nyumba
za wananchi Ngahyoma aliwataka wananchi kuepukana na kutumia vishoka na
badala yake watumie wakandarasi waliosajiliwa na Serikali kwani Tanesco
haitahusika na utapeli utakaofanywa na vishoka.
Aliwataka wateja wenye kutaka kuunganishiwa umeme kufika katika
ofisi za Tanesco na kulipia ili wataalamu wake wakague mifumo ya umeme
katika nyumba zao kabla ya kuwaunganishia na huduma ya umeme.
Akizungumzia changamoto katika utekelezaji wa mradi wa umeme
vijijini uliotekelezwa na REA Awamu ya Pili Ngahyoma alieleza kuwa ni
pamoja na wateja kudai fidia, idadi ya mahitaji ya umeme kuwa makubwa
kuliko uwezo wa mradi, na miuondombinu kama barabara kuwa mibovu hali
iliyopelekea kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi
Katika wilaya ya Shinyanga jumla ya vijiji tisa vilinufaika na
mradi wa umeme vijijini unaofadhiliwa na REA Awamu ya pili kwa gharama
ya shilingi bilioni 4.2.
No comments:
Post a Comment