Na JOHN DOTTO Mwanza
WAZIRI wa Ujenzi Dk. John
Magufuli ameagiza kufungwa kwa mfumo mpya wa kielektroniki katika vivuko
vyote nchini ili kukabiana na wajanja wachache wanahujumu mapato katika
vivuko hivyo.
Mbali ya hilo, ameagiza kufanywa
kwa utaratibu utakaowezesha huduma katika vivuko zinatolewa kwa saa 24
ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Dk. Magufuli alitoa maagizo hayo
jana katika uzinduzi wa mfumo mpya wa kielektroniki katika kivuko cha
Kigongo -busisi mkoani hapa uliowekwa na Kampuni ya Africom Tanzania.
“Tulianze pale Kigamboni na
tukaona mafanikio, tulipokuja hapa (Kigongo) tukaboresha na mafanikio
yameonekana kwa kiasi kikubwa. Vivuko vyote sasa vifungwe mfumo mpya wa
kielektroniki…vivuko vyote nchini,” aliagiza Magufuli.
Alisema mfumo huo una faida
kubwa ikiwemo kudhibiti upotevu wa mapato ambapo katika kivuko cha
kigongo – Busisi alisema mapato yameongezeka kwa takribani asilimia 40
baada ya kufungwa kwa mfumo huo.
Hata hivyo, Dk. Magufuli
alikataa kutaja ni kwa shilingi ngapi mapato hayo yameongezeka kwa hofu
kuwa watu wenye dhmira mbaya wakisikia wanaweza kwenda na kufanya
uhalifu.
Pia, aliagiza Kivuko kwa Kigamboni nacho kiboreshwe mfumo wake kama ilivyokuwa kwa Kigongo – Busisi.
Waziri huyo wa Ujenzi, alisema
kutokana na mafanikio yanayopatikana katika kudhibiti upotevu wa mapato
na kurahisisha huduma kwa wananchi, wafanyakazi husika kwa maana ya wale
wa TEMESA maslahi yao yanapaswa kuangaliwa upya na kuboreshwa.
“Kama mapato ni mazuri,
wafanyakazi nao walipwe vizuri, wasikae kimasikini kwani wanapaswa kuona
mwaka 2015 ni ukombozi katika maisha yao.
Alisema serikali chini ya
uongozi wa Rais Jakaya Kikwete imefanikiwa kujenga madaraja yote makubwa
nchini ambapo kwa sasa kuna madaraja 4880 nchini na kuwa wakati inapata
uhuru kulikuwa na madaraja mawili ambayo yalikuwa ya kuvutwa.
Mfumo wa kielektroniki katika
vivuko vya Kigamboni na Kigongo Busisi ulifungwa na Kampuni ya Africom
Tanzania ambaye Mkurugenzi Mtendaji wake Juma Rajabu alisema
watahakikisha wanafunga mifumo ambayo itadhibiti upotevu wa mapato na
kurahisisha huduma kwa wananchi ambao ndiyo watumiaji.
No comments:
Post a Comment