Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya
Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itakutana Zanzibar Januari 13, kwa
kikao cha kawaida cha siku moja chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya
Mrisho Kikwete.
Kikao hicho cha Kamati Kuu
kitatanguliwa na kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu
kitakachofanyika Januari 10, jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo CCM inalaani vikali
vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Chadema na CUF kwa viongozi wetu wa
serikali za mitaa katika maeneo kadhaa nchini ikiwemo mikoa ya Mwanza,
Dar es Salaam na Mbeya.
Vurugu hizo zilizosababisha baadhi
ya viongozi wetu kujeruhiwa zimetokea katika mkoa wa Mwanza ambapo
Ndugu Christopher Mgeta kutoka Mtaa wa Ibungilo na Ndugu Pascal Charles
wa Mtaa wa Kitangiri A katika wilaya ya Ilemela walivamiwa na kupigwa
wakati wa kuwaapisha.
Katika mkoa wa Dar es Salaam,
Ndugu Sultan Jeta wa mtaa wa Ukwamani katika jimbo la Kawe alifanyiwa
fujo na wafuasi hao na Katika Mtaa wa Msisiri A kata ya Mwananyamala
katika jimbo la Kinondoni Ndugu Juma Mbena alipigwa na kuvunjwa mkono.
Katika Manispaa ya Ilala, wafuasi
hao wa vyama vya upinzani walifanya vurugu wakati wa kuwaapisha viongozi
hao wa serikali za mitaa wilayani humo na kusababisha zoezi hilo
kuahirishwa.
Mkoani Mbeya vurugu za aina hiyo
zimetokea katika wilaya za Kyela na Rungwe ambapo wilayani Kyela zoezi
la kuapisha viongozi wa serikali za mitaa lilishindika na kuahirishwa
kutokana na vurugu za kurushiwa mawe zilizofanywa na wafuasi wa Chadema
walioletwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Katika kijiji cha Ilundo wilayani
Rungwe wafuasi hao wa Chadema waliwapiga mawe viongozi na wanachama wa
CCM na baadae kufyeka mashamba yao ya migomba na kusababisha vijana sita
kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Rungwe kwa sababu
ya hasira za kushindwa uchaguzi.
Vurugu hizi ni mwendelezo wa tabia
na mazoea ya vyama vya upinzani nchini kutoheshimu na kufuata sheria na
taratibu za nchi. Tabia hizi si za kiungwana na ni uthibitisho wa
kuharibikiwa na kufa kwa vyama vya upinzani nchini. Mara zote wamekuwa
wakikataliwa na wananchi kwa kura, wao hukataa uamuzi huo wa wananchi
kwa kufanya fujo na vitimbi. Asiye kubali kushindwa si mshindani.
Vurugu hizi sasa inatosha.
No comments:
Post a Comment