Na:Maryam Kidiko/Kijakazi Abdalla
(Maelezo Zanzibar)
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. Mohd Gharib Bilali amesema kuwa matumizi bora
ya teknolojia ya habari yatawawezesha wanafunzi kupata elimu bora kwa
urahisi.
Hayo ameyasema leo katika skuli
ya Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi Unguja wakati wa uzinduzi wa darasa
la kompyuta ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kutimiza miaka 51
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kuwa matumizi bora ya
kompyuta yatawafanya wanafunzi kuimarika vizuri kielimu wakati dunia
hivi sasa imo katika mfumo wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya
habari.
Alisema kuwa teknolojia ya habari imekuwa kwa kiwango kikubwa jambo ambalo limekuwa likichangia ukuaji wa uchumi katika Taifa
Amewashauri wanafunzi kutumia
maendeleo ya teknolojia hiyo kwa mambo yanayoweza kuwasaidia katika
maendeleo ya masomo yao na maisha ya baadae.
“Vijana itumieni teknolojia hii katika njia zilizosahihi ili iweze kuwaletea faida” alisema Dkt. Bilali. .
Amewataka wanafunzi waongeze bidii zaidi ili waweza kumudu masomo hayo na kuleta maendeleo katika jamii na nchi kwa ujumla .
Alisema kuwa matumizi ya komputa
yanarahisisha kufundisha wanafunzi kwa njia rahisi na kuweza kujifunza
mambo mbalimbali kupitia teknolojia hiyo na kupelekea kutanuka kiakili.
Aidha Dkt. Bilali ameishukuru
Serikali ya Jamhuri ya watu wa china kupitia kampuni ya ZTE kwa msaada
wa kompyuta 50 na kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inaenea kwa kiasi
kikubwa.
Dkt. Bilali amesema msaada huo
utaweza kuleta changamoto zaidi kwa wanafunzi na kuwa na wataalamu
wengi waliobora kwa maendeleo ya taifa Amesema kuwa Serikali inathamini
sana michango inayotolewa na marafiki wa maendeleo na Serikali
itahakikisha michango hiyo inakuwa na faida kubwa kwa Taifa.
Katika risala yao walimu wa skuli
ya Kiembesamaki wameiomba Serikali kuwawekea Uzio katika Eneo la skuli
pamoja na usafiri kwa walimu na Wanafunzi.
Skuli ya Kiembesamaki Sekondari
inajumla ya Wanafunzi 1,800 kwa sasa na katika sherehe za uzinduzi huo
Dkt. Bilal amechangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya maendeleo ya
skuli hiyo.
No comments:
Post a Comment