Kikosi cha Taifa Stars Maboresho
kitacheza mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ya Rwanda itakayofanyika
Januari 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mechi hiyo ni sehemu ya programu
ya Kocha Mart Nooij kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya mechi za mchujo
michuano ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN). Mechi
za mchujo za michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani
nchini Rwanda zinaanza Mei mwaka huu.
Kocha Nooij anatarajia wakati
wowote kutangaza kikosi cha timu hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager ambacho kitakusanyika Januari 18 mwaka huu jijini Dar es
Salaam, na siku moja baadaye kwenda jijini Mwanza.
TAIFA CUP WANAWAKE KUPIGWA JUMAMOSI
Mechi za kwanza za raundi ya
kwanza za mashindano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup
Wanawake) zinachezwa kesho (Januari 10 mwaka huu) kwenye miji 11 tofauti
nchini.
Katika mashindano hayo
yanayodhaminiwa na kampuni ya Proin, Geita itakuwa mwenyeji wa Kagera
(Uwanja wa Geita), Tabora itacheza na Kigoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi mjini Tabora, Simiyu na Shinyanga (Uwanja wa Simiyu), Arusha na
Manyara (Sheikh Kaluta Amri Abeid), na Kilimanjaro na Tanga (Uwanja wa
Ushirika).
Mechi nyingine ni Lindi
itaikaribisha Mtwara kwenye Uwanja wa Ilulu, Ruvuma na Njombe (Uwanja wa
Majimaji), Mbeya na Iringa (Uwanja wa Sokoine), Katavi na Rukwa (Uwanja
wa Katavi), Dodoma na Singida (Uwanja wa Jamhuri) na Pwani itakuwa
mwenyeji wa Morogoro katika Uwanja wa Mabatini.
Timu hizo zitarudiana Januari 13
mwaka huu, ambapo baada ya matokeo ya nyumbani na ugenini timu
iliyoshinda ndiyo itakayoingia hatua inayofuata ambayo pia itashirikisha
mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
Hatua hiyo, mechi zake za kwanza zitachezwa Januari 17 mwaka huu wakati zile za marudiano zitafanyika Januari 21 mwaka huu.
Baada ya hapo, hatua itakayofuata
ni robo fainali, nusu fainali na fainali ambayo ndiyo itakayotoa bingwa
wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.
KILUVYA UTD, NJOMBE BADO ZAKIMBIZA SDL
Kiluvya United ya Pwani na Njombe
Mji ya mkoani Njombe ndizo timu pekee zilizomaliza mzunguko wa kwanza wa
Ligi Daraja la Pili (SDL) kwa kushinda mechi zote katika makundi yao,
hivyo kujipatia pointi 15 kila moja.
Njombe Mji imeongoza kundi D lenye
timu za Mkamba Rangers ya Morogoro iliyofikisha pointi nane, Wenda ya
Mbeya pointi sita, Volcano FC ya Morogoro pointi sita, Town Small Boys
ya Ruvuma pointi tano na Magereza ya Iringa yenye pointi moja.
Katika kundi C, Kiluvya United
inafuatiwa na Mshikamano ya Dar es Salaam yenye pointi kumi, Abajalo pia
ya Dar es Salaam pointi saba, Cosmopolitan na Transit Camp za Dar es
Salaam ambazo kila moja imemaliza mzunguko huo ikiwa na pointi tano.
Kariakoo ya Lindi haina pointi.
Mji Mkuu (CDA) ya Dodoma na
Singida United ya Singida ndizo zinazochuana katika kundi A kila moja
ikiwa na pointi nane. Mvuvuma FC ya Kigoma yenye pointi tano ndiyo
inayofuatia, wakati Milambo ya Tabora ina pointi nne huku Ujenzi Rukwa
ikikamata mkia kwa pointi moja.
Pia mchuano mkali uko katika kundi
B ambapo JKT Rwamkoma ya Mara na Mbao FC ya Mwanza ziko kileleni kila
moja ikiwa na pointi tisa. AFC ya Arusha inafuatia kwa pointi sita,
Bulyanhulu FC ya Shinyanga ina pointi nne wakati Pamba FC ya Mwanza iko
mkiani kwa pointi moja.
Mzunguko wa pili wa ligi hiyo
itakayotoa timu nne zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza
msimu ujao (2015/2016) utaanza kutimua vumbi Januari 24 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment