Mmoja wa wakazi kutoka katika Kata
ya Nkoma iliyopo Wilayani Meatu mkoani Simiyu (kushoto) akitoa neno la
shukrani mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
(kulia) baada ya Wizara ya Nishati na Madini kusambaza umeme katika kata
hiyo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili. Kijiji cha
Nkoma ni moja ya vijiji 170 vilivyopo mkoani Simiyu vilivyofaidika na
mradi wa umeme vijijini unaotekelezwa na REA Awamu ya Pili.
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo katika moja ya mikutano
aliyoifanya katika kata za Nkoma, Balyanaga, Kabondo na Bulyashi
wilayani Meatu mkoani Simiyu.
Mtaalamu kutoka Kampuni ya LTL
(PVT) LTD inayosambaza miundombinu ya umeme vijijini katika Wilaya ya
Maswa chini ya mradi wa REA Awamu ya PIli Michael Marenye (kulia),
akifafanua hatua iliyofikiwa ya uunganishaji wa umeme katika Kata ya
Balyanaga mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
(kushoto) mara Waziri Muhongo alipofanya mkutano na wakazi wa Kata
Balyanaga ili kusikiliza kero zao.
Sehemu ya wakazi wa Kata ya
Mwambiti wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Waziri wa
Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) mara Waziri
Muhongo alipofanya mkutano na wakazi hao.
Meneja wa Shirika la Umeme Nchini
(Tanesco) Kanda ya Ziwa Mhandisi Joyce Ngahyoma akielezea namna ya
kujiunga na huduma ya umeme mbele
Na Greyson Mwase, Maswa.
Meneja Utaalamu Elekezi kutoka
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Gissima Nyamohanga amesema kuwa
serikali imetumia shilingi bilioni 881 katika mradi wa kusambaza umeme
vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya
Pili.
Nyamohanga aliyasema hayo kwenye
sherehe za uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini unaofadhiliwa na REA
uliofanyika katika kata ya Shishiyu wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Alisema kuwa Mradi wa REA Awamu
ya Pili utaiwezesha idadi ya vijiji vilivyounganishwa na umeme
3734 kati ya vijiji 15,180 ambayo ni asilimia 24.6 kufikia vijiji 5,234
ambayo ni asilimia 34.5 ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Aliongeza kuwa mradi wa REA Awamu
ya Pili wa miaka miwili ulioanza mwaka 2013, lengo lake lilikuwa ni
kuhakikisha kuwa vijiji vyote Tanzania vinapatiwa umeme hivyo kuboresha
maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi.
Akielezea mchango wa mradi wa
usambazaji wa umeme vijijini unaotekelezwa na REA katika kuboresha
maisha ya wananchi Nyamohanga alisema kuwa awali wananchi wote
walikuwa wakilipa shilingi 467,000 kama gharama ya kuunganishiwa
umeme ambayo ilikuwa ni kubwa na kupelekea wananchi wachache wenye
uwezo kuwa na nishati ya umeme huku ikiacha kundi kubwa la wasio na
uwezo kuishi gizani.
Alisema kuwa katika Awamu ya
Kwanza ya REA gharama za uunganishaji wa umeme zilishuka kutoka
shilingi 467,000 hadi shilingi 177,000 na kuongeza kuwa katika
kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uwezo wa kuunganishiwa umeme
Serikali iliamua kubeba gharama zote kupitia REA Awamu ya Pili na
wananchi kutakiwa kuchangia shilingi 27,000 tu kama kodi ya ongezeko
(VAT)
Alieleza kuwa mara baada ya
kumalizika kwa Awamu ya Pili ya REA, viongozi wataainisha vijiji
ambavyo havijapata umeme REA Awamu ya Pili, ambapo vitajumuishwa katika
mradi wa REA Awamu ya Tatu.
Nyamohanga alieleza michango
mingine kuwa ni kufungua fursa za ajira na uwekezaji kwa vijana wa
kitanzania, ufaulu kuongozeka kwa shule za sekondari na kuboreshwa kwa
huduma za afya.
“Kwa mfano kwa shughuli za
kiuchumi bei ya kusaga debe la mahindi ilikuwa ni shilingi 1,000
itashuka hadi shilingi 500 kutokana na kwamba mashine za kusaga
zitakuwa zinatumia umeme badala ya dizeli kama zamani,” alisema
Nyamohanga
Wakati huohuo Meneja wa
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Kanda ya Ziwa Mhandisi Joyce
Ngahyoma akielezea jinsi ya kuunganishwa na huduma ya umeme kwa wananchi
wa vijiji vilivyopitiwa na mradi wa REA Awamu ya Pili alisema kuwa
wananchi wanaoishi mita 30 karibu na miundombinu ya umeme
wataunganishiwa kwa shilingi 27,000 na kuwataka kuchangamkia fursa hiyo
kwa kuboresha makazi yao.
Alisema kwa wananchi wenye nyumba
zenye vyumba viwili na vioski hawahitaji kufunga mfumo wa umeme kwenye
nyumba zao (wiring) badala yake watashauriwa kununua kifaa maalumu
kijulikanacho kama “UMETA” (Umeme Tayari) kinachoweza kutumika kama
mfumo kwa kuwa na uwezo wa kuunganisha taa mbili na vifaa vingine kama
vile jiko, friji na pasi.
Aliendelea kusema kuwa kifaa hicho
kinachouzwa kwa gharama ya shilingi 37,000 kitakuwa ni mali ya mteja na
endapo atahama makazi basi atakuwa huru kuhama pamoja na kifaa chake.
No comments:
Post a Comment