………………………………………………………….
WENYEVITI wa Vijiji, Vitongoji na
Wajumbe wa Serikali za Vijiji wa Tarafa ya Moipo, Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara, wametakiwa kuwaongoza wananchi bila kuwa na upendeleo,
huba, chuki, hofu, uoga na kuficha siri za ofisi.
Wito huo umetolewa juzi na Hakimu
wa Mahakama ya Mwanzo Mirerani, Gofrey Haule, wakati akiwaapisha
wenyeviti wa vijiji, vitongoji na wajumbe wa Serikali za vijiji wa
Tarafa hiyo ili watunze siri za ofisi.
Hakimu Haule alisema ili jamii
iweze kuwaamini viongozi hao wanatakiwa kutokwenda kinyume na maadili ya
kazi, kutokwenda kinyume na utaratibu wao na bila kufanya kufanya
upendeleo wowote kwa watu watakaowaongoza.
“Uongozi ni kama kuongoza njia
hivyo mkijenga mahusiano mema kati yenu na jamii mtaweza kutekeleza
majukumu yenu bila kuwa na shaka ila msikiuke viapo vyenu kwani siyo
jambo jema mbele ya wananchi,” alisema Hakimu Haule.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi
walioapishwa waliahidi kuwa watawatumikia wananchi bila kuwa ubaguzi
wowote ule, kwani hivi sasa suala la siasa lilishapita na kilichobaki ni
kupambana na maendeleo ya jamii peke yake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Kiongoji cha Tenki la Maji, Rajab Msuya alisema wananchi wakishirikiana
naye bega kwa bega wataweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia
fikra mpya na uongozi mpya uliopo eneo hilo.
Naye, Mwenyekiti wa kitongoji cha
Kilimanjaro, Elizabeth Kisamo (Chadema) alisema atawatumikia wananchi
wote wa kitongoji chake bila ubaguzi wa itikadi, dini, kabila au jinsia,
kwani hivi sasa yeye ni kiongozi wa watu wote.
“Kwa sababu wazee ndiyo waliniomba
niongoze hiki kijiji, nitajitahidi kuongoza kwa nguvu zangu zote ila
busara zao bado ninazihitaji na waendelee kunipa ushirikiano wao,”
alisema Mussa Chully, Mwenyekiti wa Kijiji cha Shambarai.
No comments:
Post a Comment