Kaimu
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam
(DAWASA) Didas Mwilawi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha akisalimiana na
Mwenyekiti wa wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya DAWASA Christine Kilindu
alipowasili eneo zinapojengwa ofisi za mradi wa bomba kuu la maji kutoka
Ruvu Juu zilizopo Kibaha.
Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na
Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) wamefanya ziara ya siku moja katika
mikoa ya Dar es salaam na Pwani kukagua na kujionea hatua iliyofikiwa
katika mradi wa ujenzi wa miundo mbinu ya maji kutoka Ruvu Chini na Ruvu
Juu ili kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa wananchi katika
mikoa hiyo.
Ziara ya wajumbe hao wa kamati Ufundi ilianza kwa kukagua kazi
ya ukarabati wa kituo yalipo matangi ya maji eneo la Chuo Kiukuu cha Dar
es salaam, maungio ya mradi wa bomba jipya yaliyopo eneo la Mpiji,
ujenzi wa ofisi ya mradi wa bomba kuu la maji kutoka Ruvu Juu zilizopo
Kibaha, kukagua mabomba yaliyohifadhiwa eneo la Kibaha Mwendapole na
upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu Mladizi na Ruvu darajani.
Akifanya majumuisho ya ziara hiyo Mwenyekiti wa wa Kamati ya
Ufundi ya Bodi ya DAWASA Christine Kilindu amesema kuwa wajumbe
wameridhishwa na kasi ya ujenzi wa miundo mbimu hiyo ambapo matarajio
mradi huo utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa mwishoni mwa mwaka
huu.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa wananchi wa mikoa ya Dar es
salaam na Pwani watarajie kupata huduma ya maji iliyo bora mara miradi
ya Ruvu Juu Chini itakapokamilika.
Aidha, Christine amewaasa wananchi wa maeneo yanapopita mabomba
wa miradi hiyo kuyatunza vizuri kuanzia wakati huu yalipohifadhiwa na
yatakapokuwa yameanza kutumika ili yawanufaishe wananchi wote wa mikoa
hiyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi DAWASA Romanus Mwang’ingo alisema kuwa
pamoja na kuboresha huduma kwa maeneo yaliyo pembezoni mwa barabara ya
Morogoro yaani Kimara, Mbezi, Kiluvya, Kibaha, Visiga, Mlandizi na
Kibamba, utekelezaji huo pia utawanufaisha wakazi wa Ubungo, Vingunguti,
Kimara, Tabata na Kinyerezi ambao nao wanahudumiwa na mtambo unaotoa
maji kutoka Ruvu Juu.
Mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini unalenga kuongeza
uzalishaji maji na kuwahudumia wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ),
Chasimba, Buma, Zinga, Kerege, Mpiji, Bunju, Wazo, Salasala, Madale,
Kinzudi, Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani, Mikocheni,
Mlalakua, Masaki, Sinza, kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni,
Kigogo, Vingunguti, Buguruni, Kariakoo na Ilala.
Kazi hiyo ya maboresho inafanyika chini ya mpango maalumu wa
kuboresha huduma ya upatikanaji wa Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es
salaam na maeneo mengine yanayohudumiwa na DAWASA unaohususha ujenzi wa
miradi mipya na pamoja na kukarabati miundombinu iliyopo.
No comments:
Post a Comment