Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema lengo la
kuandaa Tamasha la Biashara Zanzibar ni kushajihisha ukuwaji wa Uchumi
na kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya zamani ya kuwa kituo kikuu cha
Biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amefahamisha kuwa Tamasha hilo
ambalo litawakutanisha Wafanya Biashara wakubwa kutoka Zanzibar na
sehemu nyengine litatoa fursa kwa wafanya biashara wadogo na wanunuzi
wengine wa kawaida kupata bidhaa muhimu kwa bei ya kawaida.
Hayo aliyasema wakati wa ufunguzi
wa Tamasha la Pili la Biashara la mwaka 2015 huko katika Viwanja vya
Maisara Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kutimiza
miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Wafanya Biashara na Wajasiria
Mali waitumie fursa hii adhimu ipasavyo kwa lengo la kuendeleza Biashara
hapa Zanzibar na kupata huduma muhimu”Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif alifahamisha kuwa
Matamasha ya Biashara hutoa fursa ya kukuza Sekta ya Utalii kwa
kuhudhuriwa na wageni mbali mbali kutoka nje.
Alisema nchi nyingi Duniani
zinafaidika na Matamasha makubwa ya kibiashara kama vile Tamasha la
Dubai Shoping Festival linalokusanya zaidi ya Wageni Milioni 4.4 na
kuchangia pato la Taifa zaidi ya Bilioni 15.
Alieleza kuwa Serikali itaendelea
kushirikiana na Wafanya Biashara wa Zanziba,r Tanzania na Afrika
Mashariki katika kuhakikisha sekta ya Biashara inazidi kukua na
kuimarika ili kuongeza pato la Taifa .
Sambamba na hayo alisema Serikli
itaendelea kushughulikia changamoto zinazoikabili Sekta ya Biashara
kama vile upatikanaji wa vifungashio, kuanzisha mfumo wa nambari za
utambulisho wa bidhaa (barcodes) na kufikia Viwango vya Biashara
Kimataifa.
“Ni vyema Matamasha ya aina hii
yakajumuisha maonyesho ya Utamaduni wa Mzanzibari zikiwemo kazi za
Sanaa, Vyakula vya asili na Muziki wa mwambao ambao unaendelea
kutoweka” Alisema Makamu wa Pili.
Ameitaka Wizara ya Biashara,
Viwanda na Masoko kulitangaza zaidi Tamasha la Biashara na kuanzisha
eneo maalum la maonyesho ya Biashara hapa Zanzibar.
Balozi Seif alitoa shukurani zake
kwa Taasisi za Serikali na watu binafsi, Makampuni, Wafanya Biashara
wa ndani na nje ya nchi kwa kushiriki Tamasha hilo.
Nae Waziri wa Biashara Viwanda na
Masoko Nassor Ahmed Mazurui alisema zaidi ya Wafanya Biashara 160
watashiriki Tamasha la mwaka huu.
Alisema Tamasha hilo linalengo la
kuitangaza Zanzibar Kiutalii na Kibiashara kwa kuandaa mazingira mazuri
ili kuleta kivutio kikubwa kwa washiriki na wanunuzi.
No comments:
Post a Comment