Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akitoa maelekezo kwa mtaalamu kutoka
kampuni ya Symbion iliyopewa kazi ya kujenga miundombinu ya umeme katika
kijiji cha Nyamikoma kilichopo wilayani Busega Bw. Steve Thomson
(kushoto)
………………………………………………………………………………………….
• Vijiji 1,500 kupatiwa umeme
Na Greyson Mwase, Busega
Imeelezwa kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu mradi
wa usambazaji wa umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) Awamu ya Pili kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini
(Tanesco) unatarajiwa kukamilika, ikiwa ni pamoja na kuvipatia umeme
vijiji 1,500.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo kwa nyakati tofauti alipofanya ziara katika vijiji vya Ihale,
Bukombe, Nyamikoma, Bushigwamala, Mwamagigisi, Mkula vilivyopo katika
wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Profesa Muhongo anafanya ziara katika mikoa ya Simiyu, Tabora na
Shinyanga lengo likiwa ni kukagua miradi ya umeme vijijini pamoja na
kuzungumza na wananchi.
Alisema kuwa wakandarasi wote nchini wanaotekeleza miradi ya
umeme vijijini inayotekelezwa na REA awamu ya pili kwa kushirikiana na
Tanesco wanatarajiwa kukamilisha na kukabidhi miradi yao mwishoni mwa
mwezi Juni ambapo itakuwa ni mwisho wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Profesa Muhongo alisema kuwa mara baada ya kumalizika kwa mradi
wa umeme vijijini awamu ya pili, mapema Julai Serikali inatarajia
kuingia katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa usambazaji wa nishati ya
umeme vijijini lengo likiwa ni mwendelezo wa kuboresha maisha ya
wananchi hasa waishio vijijini na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa
nchi.
Alisema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa nishati ya umeme katika
ukuaji wa uchumi wa nchi, Serikali imeelekeza nguvu zake zote katika
kusambaza umeme husasan vijijini kwa lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo
mwaka 2025 asilimia 75 ya watanzania wanapata umeme wa uhakika na hivyo
nchi kutoka katika kundi la nchi masikini duniani na kuwa nchi yenye
kipato cha kati.
Akizungumzia gharama ya uunganishaji wa umeme nchini kwa
wananchi waliopo chini ya mradi wa usambazaji wa umeme vijijini
unaotekelezwa na REA Profesa Muhongo alisema kuwa ni shilingi 27,000
ambayo ni VAT peke yake na kuwataka wananchi walio chini ya mradi huo
kuchangamkia fursa ili waweze kufaidi umeme kwa gharama ambayo ni ya
chini mno.
Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi hasa waishio
vijijini wanamudu gharama ya kuunganishiwa umeme na kujikwamua kiuchumi.
Alisisitiza kuwa kwa wananchi waliochelewa kutuma maombi yao ili
kuunganishiwa umeme chini ya mradi wa REA awamu ya pili, wasubiri awamu
zingine zinazofuata, au walipe shilingi 177,000 kwa Tanesco na
kuunganishiwa umeme muda wowote watakaohitaji
“ Kwa wale wanaohitaji kuunganishiwa umeme muda wowote na
Tanesco nje ya kutegemea miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na REA
kwa awamu watatakiwa kulipa shilingi `177,00 bila nguzo na fedha hizi
zinaweza kulipwa kwa awamu, ‘’ alisema Profesa Muhongo.
Aliendelea kufafanua kuwa awali wananchi walitakiwa kulipa
shilingi 467,000 lakini Serikali ikaamua kushusha bei hadi kufikia
shilingi 177,000 ili kuwawezesha wananchi wote kuunganishiwa umeme.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini awamu ya
tatu, Profesa Muhongo alieleza kuwa maombi yatachukuliwa nchi nzima kwa
vijiji vilivyokosa umeme katika awamu ya pili, na baada ya hapo mradi
utaanza kutekelezwa kwa vijiji vichache kwa kila mkoa, kwa awamu tofauti
lengo likiwa ni kuhakikisha panakuwepo na usawa katika kunufaika na
miradi ya umeme vijijini.
Akizungumzia gharama ya umeme nchini Profesa Muhongo alisema
kuwa gharama za umeme zinatarajiwa kushuka mara baada ya Tanesco kuanza
kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia
Alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka
Mtwara hadi jijini Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 542, na kuanza
kuzalisha gesi, kutapelekea kushuka kwa gharama za umeme kwani umeme
unaozalishwa na gesi ni nafuu kuliko umeme unaozalishwa kutokana na
mafuta mazito unaotumika sasa.
Aliongeza kuwa mbali na bomba la gesi kuchangia kushuka kwa
gharama za umeme na kupatikana kwa umeme wa uhakika, gesi hiyo
itapelekea kuongezeka kwa fursa nchini za uwekezaji nchini husan viwanda
vya mbolea, sementi na kuongezeka kwa ajira
Alisema kuwa gesi hiyo itatumika katika magari na kupikia majumbani hivyo kupunguza uharibifu wa mazingira.
Akielezea mikakati mingine ya serikali katika kuhakikisha kuwa
umeme unaopatikana unakuwa ni wa uhakika, Profesa Muhongo alisema kuwa
serikali imebuni vyanzo vingine ya nishati ya umeme kama vile makaa ya
mawe, jua, jotoardhi, bayogesi na upepo huku ikikaribisha wawekezaji
kutoka ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa nishati ya umeme
inakuwa ni ya uhakika.
No comments:
Post a Comment