Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na
Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo
akitoa taarifa ya kupungua kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Desemba,
2014 leo jijini Dar es salaam.Wengine ni Meneja wa Takwimu za Ajira na
Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja (kushoto) na Johnson Nyella, Meneja
Utafiti wa Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
………………………………………………………………..
Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
Dar es salaam.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa
mwezi Desemba 2014 umepungua hadi kufikia asilimia 4.8 kutoka asilimia
5.8 iliyokuwepo mwezi Novemba kutokana na kupungua kwa bei ya bidhaa na
huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei
wa Taifa leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za
Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa
kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula zikiwemo Mahindi, Unga wa mahindi,
mbogamboga, mihogo ,sukari ,Mafuta ya taa, dizeli, petroli na Simu za
kiganjani kumechangia kupunguza mfumuko wa bei nchini
Amesema kuwa wastani wa Mfumuko
wa Bei wa Taifa wa mwaka mzima kutoka Januari hadi Desemba 2014
umepungua hadi kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 7.9 uliokuwepo
kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2013.
Ameeleza kuwa Tanzania
inaendelea kufanya Vizuri katika nchi za Afrika Mashariki katika
kudhibiti Mfumuko wa bei kwa kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti
viashiria vinawezakuchangia kuwepo kwa mfumuko wa bei.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mfumuko
wa bei katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Kwesigabo amesema kuwa
umekuwa na mwelekeo unaofanana, Kenya ukipungua na kufikia asilimia
6.02 mwezi Desemba kutoka 6.09 za mwezi Novemba na Uganda ikiwa na
mfumuko wa bei wa asilimia 1.8 kutoka asilimia 2.1 za mwezi Novemba,
2014.
Aidha, amesema mwenendo wa
Fahirisi za bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei
za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini katika kipindi cha
mwezi Desemba 2014 amesema kuwa Fahirisi hizo zimeonyesha kuongezeka
hadi kufikia150.92 kutoka 150.54 za mwezi Novemba 2014.
Amefafanua kuwa kuongezeka kwa
Fahirisi hizo kunatokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na
bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo mchele, unga wa mahindi, samaki,
matunda jamii ya machungwa, mbogamboga, mavazi ya wanaume na wanawake na
viatu vya wanaume.
Kwa upande wake Meneja Utafiti
wa Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Johnson Nyella ameeleza kuwa
kuendelea kupungua kwa Mfumuko wa Bei nchini kunatokana na hatua
mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kupitia Benki hiyo kwa kuangalia
utekelezaji wa Sera na Mipango ya maendeleo.
Amesema kuwa katika kuhakikisha
kuwa Tanzania inaendelea kuwa na utulivu wa Uchumi kwa kipindi kirefu,
Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikifuatilia mwenendo wa bei katika Soko la
Dunia, bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini na ufuatiliaji wa
mwenendo wa uchumi wa nchi zinazoizunguka Tanzania.
Amesema malengo ya muda mrefu ya Benki kuu ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa Mfumuko wa bei unapungua na kufikia asulimia 5.
No comments:
Post a Comment