Mbunge wa Maswa Magharibi John Magale Shibuda (kushoto)
akitafsiri hotuba ya shukrani iliyotolewa kwa lugha ya kisukuma na mmoja
wa wakazi wa kijiji cha Shishiyu mbele ya Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo kabla ya kuzinduliwa rasmi kwa mradi huo.
……………………………………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Simiyu
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema
kuwa serikali imetumia shilingi bilioni 25.7 kwa ajili ya kusambaza
umeme katika vijiji 170 vilivyopo ndani ya mkoa wa Simiyu
Alisema hayo alipokuwa akizindua mradi wa umeme vijijini
uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili
iliyoanza mwaka 2013 inayotarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Juni
mwaka huu.
Akifafanua idadi ya vijiji vilivyonufaika na REA Awamu ya Pili
Profesa Muhongo alieleza kuwa katika Wilaya ya Bariadi vijiji 45
vilipatiwa umeme, katika Wilaya ya Maswa vijiji 82 vilipatiwa umeme,
katika Wilaya ya Busega vijiji 19 vilipatiwa umeme, katika Wilaya ya
Itilima vijiji 7 vilipatiwa umeme na katika Wilaya ya Meatu vijiji 17
vilipatiwa umeme.
Akizungumzia hali ya usambazaji wa umeme vijijini nchini Profesa
Muhongo alisema kuwa vijiji 3734 kati ya vijiji 15,180 ambayo ni
asilimia 24.6 vina umeme na kuongeza kuwa mara baada ya kukamilika kwa
mradi wa REA Awamu ya Pili mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu kwa
kuongeza vijiji 1500 idadi ya vijiji vyenye umeme itaongezeka na kufikia
5234 ambayo ni sawa na asilimia 34.5.
Akizungumzia gharama za uunganishaji wa umeme vijijini Profesa
Muhongo alisema kuwa katika REA Awamu ya Kwanza gharama zilishushwa
kutoka shilingi 467,000 hadi shilingi 177,000.
Alieleza kuwa katika Awamu ya Pili ya REA Serikali ilishusha bei
ya uunganishaji wa umeme bila nguzo kutoka shilingi 177,000 hadi
shilingi 27,000 ili kuwawezesha wananchi hasa waishio vijijini kuweza
kumudu gharama za uunganishaji wa umeme na kuwa na maisha bora.
Alisema mara baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme vijijini wa
REA Awamu ya Pili wananchi ambao wanahitaji umeme nje ya mradi wa REA
watalipia shilingi 177,000 tu na iwapo wataona bado wanahitaji umeme
chini ya mradi wa REA basi watatakiwa kusubiri awamu nyingine.
“ Huduma ya umeme haina itikadi ya kisiasa, kidini ni haki ya
kila mwananchi kupata umeme wa uhakika, na sisi kama Serikali
tutahakikisha kuwa tunatumia vyanzo vyote vya nishati ili kuwa na umeme
wa kutosheleza nchi nzima na kupelekea nchi kuondokana na umasikini.”
Alisema Profesa Muhongo.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa
umeme vijijini kupitia REA Awamu ya Tatu vijiji vyote nchini vitapatiwa
umeme kwa uwiano ulio sawa na kwa awamu tofauti ili kuhakikisha kila
wilaya na kijiji kinanufaika na mradi huo.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa inatokomeza
umasikini kwa watanzania kwa kuwapatia nishati ya umeme kwani ni mhimili
mkubwa wa uchumi wa nchi.
“Hakuna nchi yeyote duniani iliyoendelea bila kuwa na umeme,
tunahitaji umeme kwenye viwanda vyetu, maabara mashuleni, vituo vya afya
na katika shughuli nyingine nyingi muhimu za kiuchumi,”alisisitiza
Profesa Muhongo
Wakati huo huo Mbunge wa Bariadi Magharibi John Magale Shibuda
akizungumza kupitia hotuba yake kwenye uzinduzi wa mradi huo alitumia
fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Nishati na Madini Profesa Muhongo kama
kiongozi mchapakazi, mzalendo na mwenye kuitakia mema nchi.
Alisema pamoja na Wizara ya Nishati na Madini kukumbana na
changamoto mbalimbali lakini Waziri huyo amekuwa imara katika kutekeleza
majukumu yake kwa kusimamia vyema sekta ya nishati na madini ambayo ina
mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Natumaini ninyi mtakuwa mashahidi wangu, tukiweka tofauti za
itikadi za kisiasa, Profesa Muhongo ni mtendaji na ushahidi ni huu
usambazaji wa umeme vijijini kwa kasi ya ajabu, kwani kupitia REA Awamu
ya Pili vijiji 170 katika mkoa wa Simiyu vimeunganishwa na umeme,’’
alisisitiza Shibuda
No comments:
Post a Comment