NA RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na
watoto inaandaa zoezi la utambuzi wa wazee wenye umri kuanzia miaka 60
na kuendelea ili kutambua sehemu wanazoishi na kuwaandalia mazingira
mazuri ya maisha yao.
Akizungumza katika mkutano wa
Kamati Tendaji ya Mpango huo katika Wizara ya Uwezeshaji Mwanakwerekwe,
Mkuu wa kitengo cha Hifadhi ya Jamii Zanzibar Salum Rashid amesema zoezi
hilo litafanywa katika shehia zote za Zanzibar.
Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo
kwamba baada ya wazee hao kutambuliwa watapewa kadi maalum ambazo
zitawasaidia kwenye huduma muhimu za msingi za kijamii zinazotolewa na
Serikali zikiwemo usafiri na matibabu bila malipo.
“Lengo ni kuwaoredhesha wazee wote
waliofikia umri kuanzia miaka 60 hapa Zanzibar kujua idadi yao
kijinsia, Wilaya na Shehia zao na kuwapa vitambulisho maalum
vikavyowawezesha kupata huduma muhimu za kijamii bila malipo”
alisisitiza Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya Jamii.
Salum amesema maandalizi ya zoezi
hilo yako katika hatua nzuri na litafanywa kwa uangalifu mkubwa ili
kuhakikisha kila aliefikia umri huo aweze kuoredheshwa kupitia shehia
wanazoishi.
Katika kufanikisha mpango huo
Wizara itaandaa vijana wasiopungua 45 na kuwapa mafunzo ya kazi hiyo
na kila shehia itakuwa na kijana mmoja ambae atashirikiana na sheha
ama mjumbe wake.
Amesema kwa mujibu wa sensa ya
mwaka 2012 Zanzibar inaowazee 58311 wenye umri wa kuanzia miaka 60
ambao ni sawa na asilimia 4.5 ya wananchi wote.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa
utafiti uliofanywa na Shirika la HelpAge mwaka 2009, asilimia 60 ya
wazee wenye umri huo hawana kipato rasmi cha kuendeleza maisha yao na
baadhi yao wamekuwa wakipata msaada mdogo kutoka kwa jamaa zao.
Amesema kutokana na usumbufu wa
maisha unaowapata wazee hao ndipo Serikali ikaamua kuandaa mpango huo
ili waweze kupatiwa msaada.
Akizungumza katika mkutano huo
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana,
Wanawake na Watoto Msham Abdalla Khamis amesema zoezi hilo halina
uhusiano wowote na masuala ya siasa hivyo amewataka wananchi wasiwe na
wasi wasi .
Amesema utaratibu kama huo wa
kuwatunza na kuwasaidia wazee unafanyika katika nchi nyingi duniani na
umekuwa na mafanikio makubwa kwao.
Aidha amesema lengo kuu la mpango
huo ni kuwatambua wazee sehemu wanazoishi ili kuwasaidia waweze
kujikimu kimaisha na kuwapatia baadhi ya huduma muhimu za kijamii bila
malipo
No comments:
Post a Comment