Shirika la Ndege la Taifa la
Shelisheli, Air Seychelles limeanza kufanya safari zake kati ya mji mkuu
wa nchi hiyo, Mahe na Dar es Salaam ambapo leo, Desemba 2, 2014, ndege
yake ya abiria HM 777 ilifanya safari yake ya kwanza ya uzinduzi kwa
kutua Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Ujio wa shirika hilo la ndege
unafanya mashirika ya ndege yaliyoanzisha safari zake kuja Dar es Salaam
kwa siku za hivi karibuni kufikia matatu, Air Seychelles, Flydubai ya
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Rwandair ya Rwanda. Shirika lingine
la ndege, Etihad la Abudhabi (UAE) linatarajiwa kuanza safari zake mwaka
2015.
Uzinduzi wa safari za ndege ya Air
Seych elles ulifanywa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhandisi Dk. Charles
Tizeba na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud
Mgimwa, wabunge na viongozi kadhaa wa Serikali na wadau wa masuala ya
sekta ya usafiri wa anga na maliasili na utalii nchini.
Katika hotuba yake, Naibu Waziri
wa Uchukuzi, Mhandisi Dk. Tizeba alisema ujio wa Air Seychelles
umefungua ukurasa mpya wa safari kwa wananchi wa nchi za zisizopakana na
bahari ya Hindi (landlocked) na fursa zaidi za utalii kwani sasa
watakuwa na uhakika wa kuunganisha safari zao kwenda kokote duniani kwa
ndege hiyo.
Naibu Waziri Tizeba alisema ujio
wa ndege hiyo utakuza sekta ya utalii kati ya nchi hizo na kunufaisha
wananchi wake na kwa kujua umuhimu wa sekta ya usafiri wa anga kwa nchi
hizo, alizitaka Tanzania na Shelisheli kutekeleza mikakati ya kitaifa,
kikanda na dunia ya usafiri wa anga kuleta maendeleo ya sekta hiyo nchi
mwao.
Alitoa rai kwa wafanyabiashara ya
sekta ya utalii kutumia fursa hii kukukuza biashara kati ya nchi hizi
kwani Tanzania ina hazina ya vivutio vya utalii ikiwemo maeneo ya
kihistoria Zanzibar na Bagamoyo, mlima mrefu kuliko yote Afrika,
Kilimanjaro na moja ya maajabu saba ya dunia, Kreta ya Ngorongoro mkoani
Manyara.
Naibu Waziri Dk. Tizeba alisema,
Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha safari za ndege kati ya
Tanzania na Shelisheli zinadumu na kwamba Serikali za nchi hizo
zitahakikisha mkataba wa ushirikiano wa sekta ya usafiri unasainiwa
haraka iwezekanavyo na mamlaka husika za usafiri wa anga nchini kwa
mujibu wa masharti ya ICAO.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
Mhandisi Suleiman S. Suleiman alisema ujio wa ndege hiyo ni mafanikio
makubwa kwani unaongeza idadi ya ndege zinazotua JNIA ambapo juzi tu
ilikuja Flydubai na wanatarajia mwakani, 2015 Emirates itaongeza safari
kutoka 12 hadi 14 kwa wiki.
“Sisi (TAA) hatulali. Tunafanya
kazi kwa ushirikiano na mshauri mwelekezi wa biashara ya ndege ambaye
kazi yake ni kushawishi mashirika zaidi ya ndege kuja Tanzania. Mpaka
sasa kuna ndege 18 zinazokuja na Januari mwakani, 2015, ndege ya Etihad
inatarajiwa kuanza safari zake pia”, Mkurugenzi Mkuu huyo wa TAA
alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Meneja Mkuu wa Mahusiano wa Air Seychelles, Alan Renaud alisema safari
za ndege hiyo kati ya Mahe – Dar es Salaam zitakuza utalii na biashara
kati ya Tanzania na Shelisheli na kuwa kiungo cha safari za mashirika
mengine ya ndege duniani ambako abiria wataunganisha safari zao.
“Dar es Salaam ni njia nyingine
muhimu ya safari za ndege yetu tulizoongeza na inaonesha hatua mpya ya
kukua kwa shirika letu. Ikiwa na watu zaidi ya milioni nne na ya pili
kwa ukubwa ukanda wa bahari ya Hindi, kiungo kikubwa kwenda mbuga na
hifadhi maarufu za wanyama na vivutio vingine vya utalii kama Mlima
Kilimanjaro wenye theluji, Dar es Salaam ni chachu kubwa ya utalii na
biashara,” alisema Renaud katika hotuba yake.
Alisema, ujio wa ndege hiyo ni
matokeo ya ushirikiano mkubwa kati yao na Shirika kubwa la ndege la
Etihad Airways lenye hisa asimia 40 lililowawezesha kupata ndege ya
kwanza aina ya Airbus A320 na kuifanya Mahe kama kitovu cha abiria
kutoka Afrika Mashariki kwenda nchi za Mashariki ya Kati, Asia na za
Bara Hindi.
Air Seychelles ilianzishwa mwaka
1978 na ilianza safari za masafa marefu mwaka 1983. Kwa sasa shirika
hilo la ndege linafanya safari kwenda Abudhabi, Antananarivo
(Madagascar), Hong Kong, Johannesburg (Afrika Kusini), Mauritius, Mumbai
(India) na Paris (Ufaransa) na safari 200 za ndani mwake kwa wiki. Air
Seychellles itafanya safari zake kati ya Mahe na Dar es Salaam (JNIA)
mara mbili kwa wiki, Jumanne na Jumapili.
No comments:
Post a Comment