Na Mwandishi Wetu
MWIMBAJI wa nyimbo za injili nchini Edson Mwasabwite anayetamba
kwa sasa na kibao chake kijulikanacho kwa jina la ‘Ni kwa Neema na
Rehema’ amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la
Krismasi litakalofanyika katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Songea Desemba
mwaka huu.
Mwasabwite alisema amejipanga kikamilifu kukonga nyoyo za
mashabiki wake katika tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Desemba 25,
26 na 28 hivyo mashabiki zake wajitokeze kwa wingi kupata burudani ya
nguvu kutoka kwake.
Mwasabwite alisema mwaka huu watanzania wakae mkao wa kula kwa
kusifu na kuabudu katika Tamasha la Krismasi kwani tayari amezindua
albamu yake ya pili ijulikanayo kwa jina la ‘Asilimia mia Mungu
amenihurumia’ yenye nyimbo tisa.
“Nimejipanga vizuri kutoa burudani kwa mashabiki wangu katika
tamasha la mwaka huu la Krismasi kwani maandalizi ni mazuri, safari hii
itakuwa zaidi ya mwaka jana kwa sasa nina nyimbo nyingi zitakazowabariki
mashabiki zangu na tayari nimeshazindua albamu mpya,” alisema
Mwasabwite.
Aidha amempongeza Mkurugenzi wa Msama Promotions kwa kuweza
kuandaa Tamasha kubwa la Kikristo lenye mafanikio makubwa kwa kuweza
kuwakutanisha waimbaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa
lengo la kutangaza injili Tanzania.
“Makampuni ya Msama yanaaminika na kukubalika kwa watanzania na
nchi nyingine za jirani ndio maana hata tamasha linafanikiwa, tunaomba
wananchi waendelee kununua kazi zetu, tunaomba sapoti kutoka kwa waumini
na mashabiki wa muziki wa Injili,” alisema Mwasabwite.
No comments:
Post a Comment