Tigo Tanzania imeshinda tuzo ya “Huduma
Bora ya Kibunifu” kutokana na huduma yake ya kutuma na kupokea fedha
kimataifa kati ya Tigo Pesa Tanzania na Tigo Cash Rwanda katika
kongamano na maonyesho ya kimawasiliano barani Afrika ijulikanayo kama
AfricaCom iliyofanyika Cape Town, Afrika Kusini hivi karibuni.
Meneja Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez, alisema kwamba
tuzo hii ni matokeo ya kuwa na mwaka wenye mafanikio tele katika huduma
zake za kifedha, Tigo Pesa, ambayo imeweza kupiga hatua kubwa na
kusababisha huduma hiyo kupaa kitaifa na kimataifa.
“Ni heshima kubwa kuweza kufika kwenye sita bora na hatimaye
kuweza kunyakua ushindi wa tuzo ya AfricaCom 2014 katika Huduma Bora ya
Kibunifu. Huu ni udhihirisho tosha wa ubunifu wetu kwa ajili ya kutoa
huduma zilizo bora zaidi kwa wateja wetu wanaotumia huduma yetu ya
kutuma na kupokea fedha kupitia simu,” alisema Gutierrez wakati
akizungumza na waandishi wa habari kutoka makao makuu jijini Dar es
Salaam.
Aliongeza, “Huu umekuwa mwaka
mzuri sana kwetu katika huduma za kifedha kupitia simu. Tumeweza kuwa wa
kwanza kuanzisha na kuzindua huduma ya kwanza ya kutuma na kupokea
fedha ya kimataifa yenye uwezo wa kubadilisha moja kwa moja ankara ya
fedha kati ya Tigo Pesa na Tigo Cash Rwanda ambayo imeweza kushinda tuzo
hiyo ya AfricaCom 2014. Huduma ingine ya kwanza duniani ambayo tumeweza
kuianzisha na kuzindua mwaka huu ni gawio la Tigo Pesa kwa wateja wetu
ambao wameanza kupokea marejesho ya fedha kila baada ya miezi mine
katika akaunti zao za Tigo Pesa, ambayo imeweza kutusaidia kutimiza
wajibu wetu wa kuwajumuisha wale ambao hawajafikiwa bado na huduma za
kifedha kupitia simu.”
Huduma zingine za kibunifu ambazo
Tigo imeweza kuzindua mwaka huu pia ni ushirikiano kati ya Tigo, Airtel
na Zantel ambao inawaruhusu wateja kuweza kutuma na kupokea fedha moja
kwa moja katika akaunti za mitandao hii ya simu bila ukiritimba wowote.
Mapema mwaka huu, kampuni iliweza
kushirikiana na benki 17 nchini Tanzania ili kuwawezesha watumiaji wa
Tigo Pesa, kutuma na kupokea fedha kwa akaunti zao za benki kutoka
kwenye mifuko yao ya Tigo Pesa. Hii inawapatia wateja wetu fursa ya
kupata huduma ya kutoa na kuweka fedha kupitia Tigo Pesa na akaunti zao
za kibenki kwa masaa ishirini nan ne.
“Napenda kuwashukuru wateja wetu wa Tigo Pesa milioni 3.6 ambao
wamekuwa wakitumia huduma zetu kila siku. Wao ndio uti wa mgongo wa
motisha yetu Tigo kuweza kufanya vizuri zaidi, pamoja na kuja na huduma
za kibunifu zaidi,” alisema Gutierrez.
AfricaCom ni kongomano na maonesho ya kimawasiliano ya kila
mwaka barani Afrika. Ilifanyika Cape Town, Afrika Kusini kati ya tarehe
11 – 13 Novemba, 2014.
Tuzo za mwaka huu ziliweza kujumuisha mashindano ya tuzo 16
tofauti katika sekta ya mawasiliano kuanzia kwenye masuala ya mtandao
mpaka mambo ya masoko.
No comments:
Post a Comment