VITA dhidi ya mapambano ya vitendo
vya ukatili wa kijinsia nchini Tanzania havina budi kuungwa mkono na
makundi yote kutokana na umuhimu wake. Hali hii ni kutokana na kwamba
madhara ya ukatili katika jamii yanaathiri jamii nzima bila kujali
jinsia.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu
Mtendaji Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora –Tanzania, Bi. Mary
Massay katika Maadhimisho ya Siku 16 Kupinga Ukatili wa Kijinsia
yaliyoandaliwa na TGNP na kufanyika katika viwanja vya ofisi yao, Mabibo
jijini Dar es Salaam.
Bi. Mary Massay aliyekuwa pia
mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo ya Siku 16 Kupinga Ukatili wa
Kijinsia alisema kila jamii hainabudi kuanza kwa kuangalia mazingira
inayoishi na kuona namna gani ya kupambana na vita ya nukatili wa
kijinsia.
“…Kila mmoja analojukumu kubwa,
vyombo vya umma/dola, taasisi za umma, watu binafsi, mitandao na
wanaharkati wanajukumu kubwa katika kupambana na ukatili wa kijinsia,
huwezi kuleta maendeleo kama watu wanteseka, kwa hiyo kila kundi lina
jukumu la kupambana na ukatili wa kijinsia,” alisema Bi. Massay.
“Vita dhidi ya Ukatili wa Kijinsia
inahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa wanaanchi na viongozi ngazi zote
ili ikomeshwe. Vita dhidi ya ukatili wa kijinsia haina mwanamke wala
mwanamume, ni lazima tupate watu wa kutosha kutoka jinsi zote
watakaouangana kudai mabadiliko. Wanaume mlioko hapa ninyi ni wadau
muhimu sana katika kuleta mabadiliko chanya ya kukomesha kabisa ukatili
wa kijinsia,” alisisitiza Katibu Mtendaji huyo wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora –Tanzania.
Aliwataka wazazi wasikubali
kugeuka mawakala wa ndoa za utotoni, ambazo zimesababisha idadi kubwa ya
wanafunzi hasa wa kike kukatishwa masomo na badala yake kuhakikisha
wanatoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria kuwawajibisha wakosaji.
“…Msikubali kuzungumza na wabakaji
au wanaowatia watoto mimba nje ya mahakama, mtu akishafanya kosa
akafikishwa mbele ya sheria viachinei vyombo hivyo vifanye kazi yake,
sheria zipo na zitatumika,” alisema.
Hata hivyo alisema zipo hatua
zilizochukuliwa na Serikali kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwa ni
pamoja na kurekebisha baadhi nya sheria kandamizi na kutunga sheria mpya
zinazozingatiwa usawa wa kijinsia na haki za binadamu.
Awali akizungumza katika hafla
hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi alizitaka
mamlaka husika kuangalia namna ya kukabiliana na tatizo la ajira nchini
kwani limechania kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwa wasichana
hususan ule wa ajira zisizo na utu, usafirishaji haramu wa wasichana,
biashara ya ngono, rushwa ya ngono, ndoa za utotoni na ukatili mwingine.
“…Tunasisitiza uwepo wa mabweni ya
kutosha katika shule zote za sekondari za kata na nyigine hususan ya
wasichana ili kupunguza umbali na mazingira hatarishi kwenda shuleni.
TGNP Mtandao na GTI tumejitahidi kupambana na ukatili wa Kijinsia kwa
kutoa elimu kwa Jamii katika ngazi zote, kufanya mafunzo mbali mbali kwa
wadau mbalimbali mfano; Jeshi la polisi yakiwemo madawati ya jinsia,
viongozi wa Dini, Viongozi wa Mila, Mahakama, viongozi mbalimbali wa
serikali za mitaa, watendaji wa halmashauri, wahudumu wa afya, na
wanaharakati wa ngazi ya Jamii kupitia vituo vya taarifa na maarifa
mikoa ya Mara, Shinyanga, Morogoro, Mbeya, Dar e salaam na Pwani,”
alisema Bi. Liundi katika hotuba yake.
Maadhimisho hayo yalioambatana na
mijadala ya wazi kwa washiriki yalishirikisha makundi ya wanaharakati
mbalimbali ngazi ya jamii kutoka mikoa anuai nchini pamoja na makundi ya
wanafunzi wa kutoka jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya mjadala huo
ilikuwa “Siyumbishi, Najilinda Mnilinde” ambayo inalenga vijana kuamini
tunaamini kuwa mapambano yanahitaji nguvu kubwa na ya pamoja.
No comments:
Post a Comment