Siku ya Kimataifa ya Kujitolea
Duniani huadhimishwa tarehe 5 Desemba kila mwaka kwa lengo la kutambua
mchango wa kujitolea unaotolewa kwa ajili ya maendeleo katika jamii
tunamoishi, kitaifa na kimataifa.
Kujitolea hujumuisha hiari,
umoja, utu na kuaminiana na kunatoa fursa muhimu katika kupambana na
maradhi, ujinga, umasikini, hifadhi ya mazingira na maeneo mengi ya
kimaendeleo ambayo yanahitaji msukumo.
Aidha, kujitolea kunatoa mchango
muhimu katika kushughulikia majanga pale yanapotokea, kuimarisha umoja
katika jamii na kuboresha maisha ya watu.
Tanzania kama sehemu ya jamii ya
Kimataifa itaadhimisha siku hiyo katika katika ukumbi wa Chuo cha
Utalii kilichopo karibu na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),saa mbili
na nusu asubuhi.
Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Ushiriki na Ushirikishwaji katika kuleta maendeleo katika ngazi zote za mitaa, taifa na kimataifa.’
Katika maadhimisho hayo,
wananchi hasa vijana watashiriki katika mdahalo kuhusu umuhimu wa
kujitolea kwa ajili ya kuleta maendeleo. Aidha, kutakuwa na shuhuda na
maonyesho ya taasisi zinazoshiriki katika shughuli za kujitolea ili
kuhamasisha na kufufua moyo wa kujitolea miongoni mwa jamii.
Watanzania hususan Vijana
wanahamasishwa kuibua shughuli za kujitolea na kushiriki katika zile
zilizokwisha anzishwa ikizingatiwa kuwa wao ndiyo nguvu kazi kubwa ya
jamii.
Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo inawakaribisha wananchi wote kushiriki katika
maadhimisho hayo muhimu ili kushiriki katika mdahalo huo na kujionea
jinsi watu mbalimbali wanavyotoa mchango mkubwa katik jamii kupitia
shughuli za kujitolea.
No comments:
Post a Comment