Kwa namna ninavyoona mambo yanakwenda Watanzania tusipokuwa makini tutakuwa watu wa matukio, watu wanaoendeshwa kwa matukio, kama tukikubali hali hiyo itakuwa jambo baya sana kwa taifa letu.
Matukio kama haya huwa ni matokeo ya chanzo fulani, matukio haya huwa ni chanzo cha udhaifu wa mifumo yetu ya udhibiti pahala fulani. Kwa sababu haiwezekani jambo likishatokea ndio tuulizane ilikuwa kuwa vipi, nafuatilia mjadala wa Bunge ninaona kila anayezungumza ama anasema mtu au taasisi fulani alipaswa kujua.
Haya mambo hayakufanyika kwa kutumia mbinu za kijasusi, mbinu ambazo hutumia intelijensia ya hali ya juu kiasi kwamba hata kama ulikuwa mlinzi anayelinda lango lakini mtu akapita katika lango hilo pasina kuonekana. Jambo linaloendelea kujadiliwa bungeni wala halikutokea kwa kificho au kutumia intelijensia ya hali ya juu kufanya wanaotuhumiwa kutenda wasijulikane kwa namna yoyote, la hasha.
Hii inanipeleka katika hoja nyingine kwamba, unapoona katika nchi yenye utawala wa sheria, mchana kweupe mambo makubwa na ya kutisha hasa yale yenye nasaba na ubadhirifu wa mali ya umma yanafanyika mchana kweupe basi hatupaswi kusubiri kuona mawingu kujua mvua itanyesha.
Ninayaandika haya kwa maana ya kujifunza, hata kama tungepata Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wazuri kiasi gani, kama mifumo ya utawala wa nchi haijashonwa vema na kwa umadhubuti kikatiba kazi yao njema ingeishia katika jitihada zao za kibinadamu na kukosa usaidizi wa mifumo na taasisi za kikatiba. Binadamu kwa asili amekuwa kiumbe ambaye bila kujitungia kanuni huwa ni msumbufu kabisa, hata kama binadamu ni mwema kiasi gani, iwapo ataishi katika mazingira yasiyo na kanuni basi wema wake utakuwa hatarini kughiribika.
Katika ulimwengu wa leo utaratibu wa kuenenda katika jamii na Taifa lolote lile ni Katiba na sisi tumeamua kuandika Katiba Mpya na Bora. Ni Katiba Mpya na Bora ndiyo pekee inaweza kuwa silaha ya mwisho kuliangamiza joka ambalo limekuwa likitaga mayai kama vile Epa, Majengo ya Benki Kuu, Richmond na haya ni mayai ambayo tumeyaokota kweupe, bado hatuna hakika ya mayai ambayo joka ameyataga kwenye mashimo, vichakani na mayai ambayo joka huenda akayataga hivi karibuni tena. Sumu ya joka ni Katiba Mpya ambayo inatuwezesha wananchi kutumia mamlaka yetu kuiwajibisha Serikali, Bunge na Mahakama. Nchi ambazo zilipuuza kushughulika na joka kikatiba zimeishia kuwa mataifa yaliyoshindwa “failed states”. Tusikubali kufika huko.
Matukio ya escrow na Katiba
Nitumie pia fursa hii kutoa rai yangu kwa Watanzania kwamba, kuwa na Katiba Bora na inayotungwa na wananchi ndiyo mwarobaini wa kuziba mianya ya ubadhirifu katika Taifa letu. Kuwa na Katiba Bora ndiyo itakuwa salama yetu katika kuona wale tuliowapa dhamana wanawajibika haraka iwezekanavyo pindi tuhuma za ubadhirifu zinapotokea katika maeneo na mamlaka yao.
Sikiliza na usome pia, kwa namna ambavyo mjadala wa sakata hili umejipambanua katika Bunge letu la Jamhuri je, unadhani, viongozi wetu hawa watadiriki kwenda kutunga masharti makali na magumu ya kuwawajibisha viongozi wanafanya ubadhirifu wa mali ya umma, ilhali wao wenyewe ni viongozi wa umma wakati huo?
Nikuoneshe kidogo Rasimu ya Warioba ilisema hivi katika suala la Maadili na Miiko ya Viongozi na Watumishi wa Umma, akiwa katika kazi za ofisi au kazi binafsi au wakati amejumuika na watu wengine, atahakikisha kwamba mwenendo wake: hauruhusu kutokea mgongano wa masilahi kati ya masilahi binafsi na maslahi ya utumishi wa umma; hauhatarishi masilahi ya umma kwa ajili ya masilahi binafsi; au haushushi hadhi ya ofisi anayofanyia kazi. (2) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1), mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji kusimamia utekelezaji wa masharti yanayohusu kanuni za uongozi wa umma. (3) Wadhifa wa “Kiongozi wa umma” kama ulivyotumika katika Sehemu hii utajumuisha viongozi wa kuchaguliwa (hii inamaanisha Rais, makamu wa rais, wabunge, madiwani n.k) na kuteuliwa (Mfano, mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za Serikali n.k) kama watakavyoainishwa kwenye sheria za nchi.
Ibara hii pamoja na mambo mengine imefutiliwa mbali na Katiba Inayopendekezwa na zaidi ya yote masharti yake mahususi yakielekezwa kutungiwa sheria na Bunge. Hebu nikuulize tena, juzi ijumaa Bunge ilibidi liahirishwe baada ya wabunge kushindwa kutengeneza sentensi ya pendekezo la hatua za kuchukuliwa kwa wale ambayo wanatuhumiwa katika sakata la escrow, unadhani wabunge hawa watakaa na kutunga masharti mahususi na makali yatakayowabana na kuwawajibisha wao dhidi ya ubadhirifu ambao huenda baadhi yako wakaja kuufanya hapo baadaye? Jambo la kuhuzunisha zaidi hata ile Ibara ndogo ya 2 inayosema Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji kusimamia utekelezaji wa masharti yanayohusu kanuni za uongozi wa umma hakuna tena.
Yaani tunarudi kule kule ambako Secretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma isiyo na meno ambayo wananchi waliipigia kelele sana kwamba kuna tuhuma nyingi kuliko masuala yanayoshughulikiwa na sekretarieti hiyo na hasa hasa wananchi wakaweka msisitizo kwa wale watuhumiwa wakubwa wakubwa.
Matukio ya escrow na maadili
Masharti mahususi yafuatayo kuanzia 203(2)(b)(e) hadi (o) yamefutwa kutoka katika Rasimu ya Warioba na hayamo katika Katiba Inayopendekezwa.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya jumla ya ibara ndogo ya (1), majukumu mahususi ya Tume yatakuwa ni: (b) kufanya upekuzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine; (e) kutoa ushauri juu ya masuala ya ubadhirifu wa fedha kwa mamlaka husika; (f) kufanya upekuzi kwa kiongozi wa umma anayepewa dhamana kabla ya kuingia madarakani; (g) kutoa elimu kwa umma kuhusu maadili na miiko ya viongoziwa umma; (h) kufanya uchunguzi kwa uamuzi yake yenyewe, au baada yakupokea malalamiko kutoka kwa mtu yeyote, kutokana nakutenda au kutokutenda kwa kiongozi wa umma au mtumishi (i) yeyote wa umma, au wakala wa Serikali, ikiwa kitendo kilichotendwa au kutokutendwa ni kinyume cha maadili ya umma; (j) kumwelekeza, baada ya kupata malalamiko au itakapoona inafaa, kiongozi wa umma au mtumishi wa umma, taasisi auwakala wa serikali au chombo chochote cha umma kufanya jambo lolote linalotakiwa na sheria, kuacha, kuzuia au kusahihisha utendaji mbaya au usiyo sahihi wa majukumu yake;
(k) kutoa ushauri kuhusu kuchukuliwa hatua kiongozi wa umma au mtumishi wa umma; (l) kumwelekeza kiongozi wa umma au mtumishi wa umma, kwa mujibu wa sheria za nchi, kutoa nyaraka zinazohusiana na matumizi ya ofisi, matumizi ya fedha au mali za umma, au kutoa taarifa ya matumizi mabaya kwa Tume, kwa hatua stahiki; (m) kuomba msaada au taarifa muhimu kutoka kwa mamlaka yoyote ya Serikali au binafsi katika kutekeleza wajibu wake,na kukagua kumbukumbu muhimu na nyaraka husika; (n) kwa kuzingatia sheria, kutangaza kwa umma, mambo yote yanayohusiana na uchunguzi uliofanywa na Tume, iwapo mazingira yanaruhusu; (o) kuchunguza jambo au mazingira yoyote yanayokiuka au kusababisha ukiukaji wa maadili.
Ninapofuatilia sakata hili sishangai sana kwanini masharti haya mahususi yameondolewa na badala yake Katiba Inayopendekezwa ikasema katika ibara yake ya 231(3) kwamba “Bunge litatunga sheria kwa ajili ya utekelezaji wa masharti ya Ibara hii”.
Mtu yeyote mwenye mapenzi mema na nchi yetu na anayependa kuona tunasifika kwa vivutio vya kitalii na siyo ufisadi kwa hakika atahakikisha Katiba Inayopendekezwa inaboreshwa na kurudisha masharti haya muhimu.
Aidha, ikumbukwe kwamba ili Katiba Inayopendekezwa iboreshwe Sheria ya Kura ya Maoni inasema katika kifungu chake cha 35, kwamba Katiba Inayopendekezwa ikipata kura za “hapana” itakuwa ni fursa ya kuiboresha kabla haijapelekwa katika duru ya pili ya Kura ya Maoni.
No comments:
Post a Comment