Na Anna Nkinda – Lindi
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
amewataka wakazi wa Kata ya Ng’apa wilaya ya Lindi mjini kuchagua
viongozi waadilifu na wenye sifa ambao watawaongoza wananchi kusimamia
shughuli za maendeleo yao.
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia
wilaya ya Lindi mjini alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na wananchi
waliohudhuria mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa
Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata hiyo.
Mama Kikwete alisema kuna baadhi
ya watu wanachagua viongozi kwa ushabiki pasipo kuangalia kiongozi huyo
kama ana sifa au la, na kuwasisitiza wananchi hao siku ya uchaguzi
ikifika wasifuate mambo ya ushabiki na kuchagua kiongozi kwani ushabiki
hauna manufaa yoyote.
“Nawaombeni muwapigie kura za
ndiyo viongozi wote wa CCM wanaogombea nafasi za Wenyeviti na Wajumbe
wa Serikali za Mitaa, kwani hawa wanasifa na mkiwachagua kutakuwa na
manufaa kwenu na vizazi vyenu hivyo basi wote mliojiandikisha siku ya
uchaguzi ikifika mjitokeze kupiga kura na kukichagua Chama chetu”,
alisema .
Aidha MNEC huyo aliwakumbusha
wanachama wa CCM siku ya uchaguzi kutokwenda kupiga kura wakiwa wamevaa
sare za Chama au mavazi yoyote yenye kuonyesha ushabiki wa Chama cha
siasa hiyo hairuhusiwi na kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Maadili
ya vyama vya Siasa na Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi .
Kuhusu elimu Mama Kikwete alisema
Serikali ya CCM kwa kushirikiana na wananchi imefanikiwa kujenga shule
za Sekondari nchi nzima na ifikapo mwakani maabara kwa ajili ya masomo
ya sayansi katika shule hizo zitakuwa zimekamilika na kuanza kutumika.
Alisema, “Ninawaomba wazazi na
walezi msimamie watoto waende shule ili wawe na maisha bora hapo baadaye
kwani tatizo kubwa lililoko hapa ni watoto kutokwenda shule. Serikali
imewajengea shule na maabara lakini kama watoto wenu hawataenda shule
ni kazi bure, ili shule hizi ziwe na faida kwenu ni lazima watoto wenu
wasome”.
Mama Kikwete pia alitembelea Kata
ya Makonde na kuongea na wanachama pamoja na wagombea wa nafasi za
Uenyeviti na Wajumbe na kuwapongeza viongozi wa zamani ambao wanamaliza
kipindi chao cha uongozi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutekeleza na
kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Aliwapongeza wanawake
waliojitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi jambo ambalo
litawawezesha kuingia katika ngazi ya maamuzi.
Mama Kikwete yupo wilayani humo
kwa ajili ya shughuli za kichama ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye
kampeni na kuwanadi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi mbalimbali
za uongozi katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na
Vitongoji utakaofanyika tarehe 14 mwezi huu.
No comments:
Post a Comment