Mechi ya Nani Mtani Jembe 2 kati
ya Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itachezwa
Jumamosi, Disemba 13, 2014 saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam, Meneja Udhamini wa TBL, George Kavishe
amesema kwamba “Tayari Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza
mechi ya Nani Mtani Jembe 2 (Nani Mtani Jembe 2 Match). Pambano hili ni
zawadi ya kufungia mwaka kwa mashabiki na kila timu imetia saini
makubaliano kwamba itachezesha kikosi cha kwanza ili kuwapa mashabiki
burudani ya uhakika.”
Kavishe aliongeza kuwa mechi hii
ni maalumu kwa ajili ya kuhitimisha kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 ambayo
imeendeshwa kwa zaidi ya miezi miwili ikiwapa fursa mashabiki wa timu
hizi kuchangia timu zao kila wanapoburudika na bia ya Kilimanjaro
Premium Lager.
Alisema Nani Mtani Jembe 2
inahusisha mashabiki wa klabu za Simba na Yanga ambapo zawadi ya
shilingi milioni 100 itatolewa na kugawanywa ifuatavyo.
Shilingi Milioni 20 ni zawadi ya
mechi ya Nani Mtani Jembe ambapo timu itakayoshinda itapata sh milioni
15 na timu itakayofungwa itapata shilingi milioni 5.
Kampeni hii inaendeshwa kwa njia ya sms ambapo mashabiki
wanapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80 zimegawanywa kati
ya timu hizo mbili ambapo kila timu ilianza na shillingi milioni 40
kwenye benki maalumu mtandaoni.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro
Premium Lager, Pamela Kikuli alisema mashabiki wa Simba na Yanga
wanaweza kushiriki kwa kununua bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye
ujazo wa mililita 500 ambapo mteja atabandua ganda la kizibo cha bia ya
Kilimanjaro Premium Lager na kuona namba maalumu. Ataandika jina la timu
yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo ya kwenye kizibo ambayo
anatuma kwenda namba 15415 na kwa kufanya hivyo anakuwa amepunguza pesa
taslimu shilingi 10,000 kutoka timu pinzani na kuichangia timu yake.
Kikuli pia alizikabidhi timu hizo
jezi maalumu itakayovaliwa mahususi kwa ajili ya mechi hiyo na
kuwahimiza mashabiki waendelee kuzipigia kura timu zao na kikubwa
kuhakikisha wanafika uwanja wa taifa na kujionea wenyewe pambano hilo
ambalo lazima mshindi apatikane.
Mkurugenzi wa Mashindano wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura
aliwakaribisha mashabiki na kuwaomba wajitokeze kwa wingi kwani hivi
sasa timu hizo ziko kambini zikijiandaa na mtanage huo wa kukata na
shoka unaotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa.
Alitaja viingilio vya mechi hiyo
kuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP B, 20,000/= VIP C, 15,000/= kwa viti vya
rangi ya chungwa kiingilio kitakuwa ni sh 15,000 huku viti vya bluu na
kijani tiketi zikiuzwa kwa sh. 7,000/=.
Wambura alisema pambano hilo
litakalosimamiwa na TFF litaanza saa kumi kamili na litachezwa kwa
dakika 90 tu ambapo kama muda huo timu hizo hazitafungana basi mikwaju
ya penati itapigwa ili mshindi apatikane.
Taji la Nani Mtani Jembe linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1 katika mechi iliyochezwa Disemba 21, 2013.
No comments:
Post a Comment