Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imetupa rufani ya timu ya Mwanza kupinga uhalali wa
wachezaji wawili wa Kigoma kwenye mechi yao ya robo fainali iliyochezwa
jana (Januari 26 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.Mwanza
iliyopoteza mechi hiyo kwa mabao 2-1 iliwalalamikia wachezaji Neema
Sanga na Vene Dickson wa Kigoma kuwa waliwahi kuchezea timu ya Taifa
(Twiga Stars), hivyo kucheza mashindano ya Kombe la Taifa la Wanawake ni
kinyume cha kanuni. Kamati baada ya kupitia rufani hiyo, imeitupa kwa
vile timu ya Mwanza haikuwasilisha vielelezo vyovyote kuthibitisha madai
hayo dhidi ya wachezaji hao. Pia Kamati yenyewe ilipitia taarifa za
Twiga Stars ambapo haikupata kumbukumbu za wachezaji hao katika timu
hiyo. Pia Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imesikitishwa na
kitendo cha viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania
(TWFA) Mkoa wa Mwanza kugomea uamuzi dhidi ya rufani yao, hivyo
imependekeza Mwenyekiti wa TWFA Mwanza, Sophia Tigalyoma na Katibu wake
Hawa Bajanguo wapelekwe Kamati ya Nidhamu kwa hatua za kinidhamu.
WASHINDI COPA COCA-COLA WAKABIDHIWA VITITA VYAO
Washindi wa Copa Coca-Cola 2014
wamekabidhiwa zawadi zao za fedha kutoka kwa mdhamini wa michuano hiyo
ya umri chini ya miaka 15 kwa wavulana na wasichana kampuni ya
Coca-Cola. Fedha hizo kwa washindi mbalimbali tayari zimeingizwa kwenye
akaunti zao.
Kwa upande wa wavulana; washindi
na kiwango walichopata ni mabingwa Dodoma (sh. milioni nane), makamu
bingwa Kinondoni (sh. milioni tano), mshindi wa tatu Kigoma (sh. milioni
tatu) wakati timu yenye nidhamu Tanga (sh. milioni moja).
Mchezaji bora Mwami Ismail kutoka
Kigoma (sh. 500,000), mfungaji bora Timoth Timoth wa Dodoma (sh.
500,000), kipa bora Kelvin Deogratia wa Geita (sh. 500,000) na mwamuzi
bora Abdallah Mbarome kutoka Zanzibar sh. 500,000).
Kwa upande wa wasichana ni
mabingwa Kinondoni (sh. milioni tano), makamu bingwa Ilala (sh. milioni
tatu), mshindi wa watatu Temeke (sh. milioni mbili) wakati timu yenye
nidhamu Mbeya imepata sh. milioni moja).
Zubeda Mohamed wa Kinondoni ambaye
ndiye mchezaji bora amepata sh. 500,000, mfungaji bora Stumai Abdallah
wa Temeke sh. 500,000 wakati kipa bora ni Suleta Saad wa Zanzibar sh.
500,000.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment