Na
Abdula Ali Maelezo-Zanzibar .
Naibu
waziri wa afya Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema Serikali haiwazarau Wakunga
wa Jadi na badala yake imeamua kuwapatia vibali maalumu ambavyo
vitawahalalishia ufanyaji wa kazi zao bila ya usumbufu ili kuokoa vifo vya
akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.
Hayo
ameyasema katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi
Unguja wakati akijibu swali la mwakilishi wa kuteuliwa wa Nafasi Maalumu za Wanawake
Mhe. Panya Ali Abdalla.
Naibu
Waziri huyo amesema kuwa Wakunga hao watapewa vibali hivyo baada ya kupatiwa
mafunzo maalumu na kuhitimu vizuri katika ngazi ya uzalishaji (Ukunga) na
kutanabahisha kuwa Wakunga hao wana umuhimu mkubwa katika jamii kutokana na
kazi yao hiyo muhimu na hususan kwa akina mama wajawazito ambao wanatarajia
kujifungua.
Amefafanua
kuwa lengo la Serikali la kuwapa mafunzo wakunga hao ni kupunguza vifo vya akina mama wajawazito ambao husumbuka
kwa kutembea masafa marefu kutafuta huduma ya kujifungua na anaamini kuwa
kutokana na elimu watakayopewa wakunga hao watasaidia kina mama hao kujifungua
salama bila ya kusumbuka kwa kutembea masafa marefu.
“Mara
nyingi vifo hivi huchangiwa na kuchelewa kwa mama mjamzito kufika katika Kituo cha
huduma kitu ambacho kinapelekea kukosa huduma ya haraka”, alieleza Naibu Wazir
Thabit Kombo.
Naibu
Wazir Thabit Kombo ametanabahisha kuwa suala la kupunguza vifo vya kina mama
vinavyotokana na Uzazi ni moja kati ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika Sekta
ya Afya na ili kupunguza tatizo hilo serikali inahitaji mashirikiano ya pamoja
kati ya Wizara ya Afya, Jamii na Sekta nyengine.
Amesema
jamii ina wajibu mkubwa katika kukabiliana na tatizo hilo kwa kufanya maamuzi
ya haraka wakati mama mjamzito anapohisi dalili za kutaka kujifungua ili kuokoa
uhai wa mama huyo na mtoto, kwani vifo vya uzazi hushuka na kupanda kati ya Mwaka
hadi Mwaka, takwimu za vifo zinaonesha kuwa Mwaka 2011 vifo 77 vilitokea na
kushuka hadi vifo 62 Mwaka 2012 na baadae kupanda tena Mwaka 2013 ambapo vifo
103 viliripotiwa kutokea na vifo 80 kwa Mwaka 2014.
Amesema
kutokana na vifo hivyo Wizara yake imechukua hatua mbalimbali katika
kuhakikisha tatizo hilo linapungua kadri itakavyowezekana, ikiwemo kupeleka
huduma ya kujifungua karibu na wananchi, kuongeza wahudumu wa afya ya uzazi katika
vituo vinavyotoa huduma hiyo, kuandaa mpango maalumu wa upatikanaji wa dawa na
vifaa vya akina mama na watoto.
Akielezea
hatua nyengine Mhe. Thabit Kombo amesema Serikali imeanzisha mpango wa
kusomesha masomo ya juu yanayohusu kina mama na watoto (Obstetrics and Gynaecology,
Peadiatrics and Child Health Care, Neonatology), kuendelea kutoa elimu kwa
akina mama juu ya umuhimu wa kuhudhuria katika vituo vya afya mapema ili
kugundua matatizo kwa wakati na kuyafanyia kazi kwa wakati unaostahiki, na
kuendelea kushirikiana na Wakunga wa Jadi ili kuwapeleka akina mama katika
vituo vya afya na Hospitali kwa ajili ya kujifungua.
Amefafanua
kuwa sambamba na jitihada hizo wizara yake imepanga mpango maalumu wa kujadili
kila kifo kinachotokea (Maternal Death Audit) ili kujua sababu ya kifo cha mama
huyo na kuweza kujipanga ili kifo kama hicho kisitokee tena pale inapowezekana.
IMETOLEWA
NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment