Tuzo
za bodi yenye uongozi bora katika sekta ya kibenki na bima zijulikanazo
kama Best Board Leadership Awards (BBLA) zinatarajiwa kufanyika jijini
Dar es Salaam kesho, ambapo taasisi saba zitashiriki katika tuzo hizo.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam hapo jana, Mratibu wa tuzo hizo, Bi. Neema Gerald,
amezitaja benki zilizothibitisha kushiriki katika tuzo hizo kuwa ni
pamoja na Benki ya Posta (TPB), Benki ya Exim na Benki ya CRDB.
“Kwa
upande wa makampuni ya bima, watakaoshiriki ni Heritage Insurance,
Alliance Insurance Corporation, Alliance Life Assurance na Strategis
Insurance (T) Limited,” alisema.
Kwa
mujibu wa Bi. Neema, tuzo hizo maalum kwa ajili ya sekta za kibenki na
bima ni mpango pekee uliopo unaolenga kutambua mchango wa uongozi bora
wa Bodi za Wakurugenzi katika sekta hizo mbili.
“Ningependa
kutoa shukrani zangu za dhati kwa makampuni yaliyoonyesha mwamko wa
kushiriki. Tuzo hizi zinalenga kutambua mchango mkubwa unaotolewa na
kundi la watu waliokabidhiwa dhamana ya kufanya maamuzi kwa niaba ya
wanahisa,” alisema.
Kwa mujibu wa mratibu huyo, Tuzo hizi zitatoa fursa
ya ufahamu ni kwa jinsi gani bodi bora inaweza kusaidia taasisi kupata
mafanikio na kufikia utendaji bora hususani katika eneo walilobobea
kiutalaam.
"Tumeona
umuhimu wa kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na wakurugenzi wa
bodi katika taasisi zao. Tunaamini kuwa katika kila mafanikio ya taasisi
ya kifedha, nyuma yake kuna bodi ya wakurugenzi imara na makini. Sasa,
sifa hizi ambazo wajumbe wa bodi wengi wanakua nazo zinapaswa
kutambuliwa na kuthaminiwa, " alisema.
Akizungumzia tuzo hizo, Bw. Laurence Mwangoka, Meneja Mauzo wa Hoteli ya Serena, ambayo ni moja kati ya wadhamini, alisema kuwa
tuzo hizo zimeanzishwa wakati muafaka nchini kipindi ambapo sekta za
Bima na kibenki zinapitia mabadiliko makubwa katika ukuaji wake.
Mbali
na Hoteli ya Serena, wadhamini wengine wa tukio hilo la kipekee ni
pamoja na Excel Management and Outsourcing, Fix Agency Ltd, IPP Media,Real
PR Solutions, Lilacnshades, Afrimax Strategic Partnerships Limited na
Capital Plus International huku wadhamini zaidi wakiaswa kujitokeza.
No comments:
Post a Comment