Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania linapenda kutoa taarifa kwa wananchi na Vyombo vya Habari
kuhusu mgogoro wa eneo la TONDORONI lililopo katika Wilaya ya Kisarawe
kama ilivyokaririwa na baadhi ya Vyombo vya Habari hapa nchini.
Taarifa zilizotolewa na
kukaririwa na baadhi ya Vyombo vya Habari kwamba Wanajeshi wametumia
nguvu kuwatoa wananchi eneo la TONDORONI na baadhi yao kudai kupotelewa
na mali zao siyo za kweli na ni za kuwapotosha wananchi kwa sababu
wananchi hao walitaarifiwa kuondoka kupitia uongozi wa Wilaya na uongozi
wa Vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B. Aidha, walipewa muda wa kutoa
vitu vyao na wao kuondoka.
JWTZ linapenda kuwahakikishia
wananchi kuwa hatua ya kuwaondoa wananchi wavamizi kutoka katika eneo la
kambi ya Jeshi kwa uangalifu, umakini na kulikuwa na usimamizi wa hali
ya juu na hakuna mali ya mwananchi iliyoporwa kama ilivyodaiwa.
Ifahamike kwamba; Jeshi linaona ni bora lilaumiwe kwa kuwaondoa wananchi
waliovamia maeneo hatarishi ya jeshi ambayo hutumika katika mafunzo
yanayohusisha risasi za moto, zana hatari za kijeshi na mabomu ambayo
wakati mwingine hulipuka baada ya muda fulani kupita badala ya kuwaacha
wakae katika maeneo hayo kutokana na sababu za kisiasa au ushabiki
mwingineo na hivyo kuwa katika hatari ya kuweza kuumia vibaya au
kupoteza maisha yao na mali zao.
Pia ni vema tukajua historia ya tatizo hili.
Mnamo mwaka 1978 eneo
linalojumuisha vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B na kilichokuwa kijiji
cha TONDORONI lilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya JWTZ.
Baada ya maamuzi hayo Kikosi cha JWTZ kilihamia TONDORONI mwaka 1981na
kukalia eneo la hekta 4197. Serikali ililipima eneo la TONDORONI
kisheria mwaka 1984 na eneo lote liliwekewa mawe ya mipaka.
Baada ya hapo, Serikali ilifanya
tathimini ya malipo kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ilikuwa mwaka
1987/88 na wakati huo kulikuwa na wananchi wapatao 1,508. Awamu ya pili
ilifanyika 1992/93 ambayo ilijumuisha tathmini ya nyumba na majengo
ambapo wananchi wengine 955 walifanyiwa tathimini.
Kufuatia tathimini iliyofanyika malipo yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwaka 1996 malipo yalifanyika kwa barua kumbukumbu Na. FE 98/371/01/73 ya tarehe 11 Juni 2003.
Malipo mengine yalifanyika
mwaka 2002 na 2006. Baada ya Malipo hayo, mengine tena yalifanyika mwaka
2012 kutokana na kesi ya madai Na. 144/1996. Kwa hiyo madai ya msingi
ya wananchi yalishalipwa na sheria ya uchukuaji ardhi imetekelezwa
kikamilifu.
Hata hivyo, mwaka 2005 baadhi ya
wananchi wachache walifungua kesi Na. 78/2005 ambayo baadae ilifutwa na
mahakama. Tarehe 10 Dec 2013 M/kiti wa kamati ya Ulinzi ya Wilaya
Kisarawe alikwenda eneo la TONDORONI kuwasomea wananchi maamuzi ya
mahakama akiandamana na mwanasheria wa Wilaya ya Kisarawe.
Pamoja na taarifa hizo kupitia
uongozi wa Wilaya na uongozi wa Vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B.
wananchi wachache wameendelea na kazi zinazochangia kuharibu mazingira
hasa ukataji wa miti, uchomaji wa mkaa na kuwasha moto mara kwa mara
hali inayotishia usalama wa kambi na wa wananchi wenyewe ikizingatiwa
kwamba hili ni eneo la mafunzo ambapo risasi za moto hutumika sambamba
na zana zingine hatari za kijeshi katika eneo hilo.
Wananchi waliowengi wanajua
ukweli kuwa eneo la TONDORONI linamilikiwa kihalali na JWTZ, lakini wapo
wananchi wachache wamekuwa wakiingia kinyemela katika eneo hilo na
kufanya ujenzi mpya usiku licha ya jitihada mbalimbali zinazofanyika
kuwaelimisha na kuwashauri kuwa waache tabia hiyo ya kulivamia eneo hilo
la Jeshi, jambo ambalo hugunduliwa na kuzuiliwa uendelezaji wa ujenzi
huo.
Jeshi linawataka wananchi
wachache wanaovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi ya
kijeshi; kutambua kuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria lakini pia kwa
mara nyingine tena kuendelea kuwakumbusha wananchi kuhusu madhara
yanayoweza kuwapata wananchi wanaovamia maeneo ya Jeshi na kujenga
katika maeneo hayo.
Jeshi litaendelea kushirikiana
na wananchi wema na kuheshimu mipaka iliyopo baina ya makambi yake na
maeneo ya wananchi lakini pia litaendelea kuwaondoa wale wachache
wanaojenga katika maeneo yake kinyume cha utaratibu.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
No comments:
Post a Comment