Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau akifafanua jambo kwa
wageni waliohudhuria hafla fupi ya kusaini mkataba kati ya shirika hilo
na timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid wa kuanzishwa kwa kituo cha
michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Dk. Dau alisema katika uendeshaji wa kituo hicho, Real Madrid itakua na
dhamana ya kushughulikia masuala yote ya ufundi, kuwatambua wachezaji,
chakula, wataalamu wa saikolojia na wataalamu wa viungo na kwamba wajibu
wa shirika lake utakuwa kwenye kujenga tu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau (aliyekaa kushoto) na
Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben
De la Red Gutierrez (aliyekaa kulia) kwa pamoja wakisaini mkataba wa
kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la
Kigamboni jijini Dar es Salaam. Wakishuhudia ni wawakilishi kutoka pande
hizo mbili. Kituo hicho kitakua na uwezo wa kupokea wanafunzi 108 kwa
wakati mmoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau (kushoto) na Mkurugenzi wa
Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red
Gutierrez (kulia) wakibadilishana mikataba ya kuanzishwa kwa kituo cha
michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Wakishuhudia ni wawakilishi kutoka pande hizo mbili. Kituo hicho kitakua
na uwezo wa kupokea wanafunzi 108 kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya
mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez akifafanua
jambo kwa wageni waliohudhuria hafla fupi ya kusaini mkataba kati ya
timu yake na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa kuanzishwa kwa kituo
cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es
Salaam. Kituo hicho kitahusisha wanafunzi 108 watakaogawanywa kwenye
timu za chini ya umri wa miaka 13, 15, 17, 19, kikosi cha pili na timu
ya wakubwa.
…………………………………………………
Na Mwandishi wetu
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) limeingia mkataba na klabu maarufu duniani ya Real Madrid
ya Hispania wa kujenga kituo cha michezo kwa ajili ya kuzalisha vipaji.
Akizungumza katika hafla ya
kusaini mkataba huo wa miaka 18, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa
NSSF, Dk Ramadhani Dau alisema ujenzi huo utagharimu Sh bilioni 16 na
unatarajiwa kuanza kujengwa Mei mwaka huu na kwamba utakamilika baada ya
miezi 18.
Dk Dau alisema kituo hicho ambacho
kitajengwa kwenye kijiji cha michezo cha shirika hilo (NSSF Sports
City), kitakuwa eneo la Mwasoga, Kigamboni, Dar es Salaam.
“Tuna eneo la zaidi ya ekari 400
ambapo tutajenga viwanja, shule ya michezo, nyumba za kuishi na maduka.
Lengo letu tuzalishe na kuuza wachezaji. Tunakusudia kuwa na timu ya
vijana chini ya umri wa miaka 13, 18, 20, timu B na timu ya wakubwa,”
alisema Dk Dau.
Alisema utekelezaji wa kituo hicho utaanza hivi karibuni kwa kutumia majengo ya kukodi wakati wakisubiri ujenzi kukamilika.
“Hivi hapa baada ya kusaini
mkataba, utekelezaji utaanza kwa kutumia majengo ya kukodi ambayo
tunadhani yatakuwa maeneo ya Temeke na tutakuwa tukitumia viwanja vya
Karume na Uhuru,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF
alisema katika kuendesha kituo hicho, kila kitu kitafanywa na Real
Madrid kuanzia masuala yote ya ufundi, kuwatambua wachezaji, chakula,
wataalamu wa saikolojia na wataalamu wa viungo na kwamba wajibu wa
shirika lake utakuwa kwenye kujenga tu.
“Sisi tunachukulia huu mradi ni
uwekezaji na hatufanyi hisani, itazingatia misingi ya biashara na faida
kubwa ni kwamba NSSF itaongeza kipato, lakini pia kituo kitatumika
kuitangaza Tanzania kwa sababu yatakayofanyika yataoneshwa kwenye
televisheni ya Real Madrid,” alifafanua Dk Dau.
“Lakini pia wakati umefika sasa
kwa Tanzania kushiriki Kombe la Dunia Qatar 2022, kama unaandaa vizuri
vijana wa miaka 13 sasa mpaka mwaka 2020 wanaweza kuwakilisha vizuri
kwenye mechi za kufuzu na mwaka 2022 wakashiriki Kombe la Dunia,
wakikosa la Qatar, basi hata hizo zinazokuja, hiyo pia ni moja ya
madhumuni ya kituo hicho.”
Akizungumzia namna walivyofikia
uamuzi wa kujenga kituo, Dk Dau alisema wazo hilo lilipatikana Agosti
mwaka jana na kisha likapelekwa kwenye Mkutano wa Wanachama uliofanyika
Arusha ambako waliazimia NSSF iwekeze rasmi kwenye michezo kabla ya
kuwasilishwa kwenye bodi na utekelezaji kuanza kufanyika.
“Tulitembelea sehemu nyingi kuona
wenzetu wanafanyaje. Binafsi nilitembelea nchi kadhaa za Ulaya, nilienda
kituo cha Manchester United, Sunderland, Real Madrid kwa hapa Afrika
nilikwenda Asec Mimosas (Ivory Coast) na TP Mazembe (Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo, DRC) kuona wanafanyaje, ziara ikazaa matunda
kwani tulikubaliana na Madrid na ndio wamekuja kusaini mkataba leo
(jana),” alifafanua Dk Dau.
Naye Mkuu wa Vituo vya Michezo wa
Real Madrid, Rayco Garcia aliishukuru NSSF wa kuwa na mpango huo na
kuahidi kufanya kazi ili kuipatia Tanzania mafanikio.
“Tukifanikiwa kuwatoa vijana hao,
Tanzania itaweza kushiriki kwenye michuano mikubwa kama alivyosema Dk
Dau, inabidi tufanye kazi ili vijana wafanikiwe, wafike mbali,” alisema
Garcia.
Mbali na Garcia ambaye pia ni
kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18 ya Madrid, wengine
walioambatana kwenye msafara huo ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu hiyo,
Ruben de la Red, Kocha Mkuu wa timu za vijana, Francisco Martin Ramos na
Juan Jose San Roman Milla. Mwaka jana, wachezaji wa zamani wa Real
Madrid walifanya ziara nchini.
No comments:
Post a Comment