Na Maryam Kidiko/
Kijakazi Abdallah –
Maelezo Zanzibar .
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imesema Kuna umuhimu mkubwa Zanzibar kuwa na Afisa muandamizi wa cheo
cha Naibu Kamishna wa Mamlaka wa Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la
kusimamia ukusanyaji wa Mapato yatokanayo na ushuru wa Fedha na ushuru
wa bidhaa katika juhudi za kuimarisha shughuli za uchumi wa Zanzibar.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Fedha
Omar Yussuf Mzee wakati akijibu suali la Mh, Jaku Hashim Ayoub Jimbo la
Muyuni alietaka kujua kama kuna ulazima wowote wa TRA kuwa na Afisa
muandamizi wa cheo hicho Zanzibar.
Amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania
ni Taasisi ya Muungano iliyoundwa kwa mujibu wa sheria Na.11 ya mwaka
1985 ambapo inapaswa kuwa na Ofisi yake Zanzibar.
Amesema kuwa kazi ya TRA Zanzibar
nikukusanya Mapato ya Muungano yanayotokana na kodi ya Mapato, Ushuru
wa Fordha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini kama
ilivyoainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977.
Ameongeza kuwa kodi itokanayo na
ushuru wa Forodha inasimamiwa na Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki ya 2004 na kwa mujibu wa sheria hiyo Zanzibar ni
sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni moja kati ya sehemu
ya nchi wanachma wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Waziri wa Fedha alieleza kuwa
sheria ya ushuru ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki imeweka
utaratibu wa uwekaji thamani Bidhaa zinazotoka Nje na Ndani ya Nchi ya
Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Amesema kwa vile Zanzibar ni
kisiwa kutumia Viwango vya Kodi moja kunaweza kuathiri Uchumi wake
hivyo Serikali imeweka utaratibu wa viwango vya kodi tofauti kama
ilivyoainiswa katika sheria ya ushuru wa Forodha wa bidhaa zinazoingizwa
Zanzibar kwa madhumuni ya soko na matumizi ya ndani
Jumla ya skuli ishirini na moja
(21) za sekondari zimejengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzinar kwa
kushirikiana na Benki ya Dunia na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya
Afrika (Badea)
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Amali Mh. Zahra Ali Hamad ameeleza hayo katika ukumbi wa Baraza la
Wawakilshi Chukwani wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Rahaleo
Nassor Salim Ali aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kujenga
majengo mapya ya kisasa ya ghorofa katika skuli ya Mwembeshauri
iliyondani ya Jimbo lake kama bado upo.
Bi. Zahra amemuhakikishia
Mwakilishi huyo kwamba mpango wa kujenga skuli ya ghorofa katika eneo la
skuli hiyo upo kutokana na kubainika kuwepo kwa idadi kubwa ya
wanafunzi katika mitaa ya karibu na skuli hiyo.
Alisema kuwa mbali na utekelezaji
wa mpango huo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na
mfuko wa OPEC inakusudia kujenga skuli kumi 10 za ghorofa ambapo mradi
huo ulichelewa kuanza kutokana na kutokamilika taratibu za kisheria
kuhusu makubaliano ya mkopo.
Wakati huo huo Wizara ya Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati inakusudia kumaliza tatizo la upatikanaji wa
huduma za maji ifikapo mwaka 2017 kwa Wananchi wa Mji mkogwe na Ng’ambu.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri
wa wizara hiyo Mh. Haji Mwadini Makame wakati akijibu suali la
Muwakilishi Ali Salum Haji (Jimbo la Kwahani) alitaka kujua juhudi za
serikali za kuondoa tatizo hilo linalowakabili wananchi wengi hasa
sehemu za mjini.
Amesema kuwa wanakusudia kumaliza
tatizo kwa kuimarisha huduma hiyo kwa kuimarisha miundo mbinu ikiwemo
kubadilisha Mabomba ya zamani ambayo yamechoka na kushindwa kuhimili
ongezeko kubwa la wahamiaji.
Aidha alisema kuwa hali ya
upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mjini inaendelea kuimarika siku hadi
siku ambapo kuna baadhi ya maeneo yanapata Maji kwa muda mrefu na
mengine yanapata maji kwa mgao hasa wakati wa kiangazi na maeneo
machache hukosa kabisa.
Alisema kupitia Mamlaka ya maji
wamekuwa wakifanya juhudi kutafuta ufumbuzi wa suala hilo ikiwa ni
pamoja na uchimbaji wa Visima vipya katika maeneo mbali
mbali.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment