Sehemu ya Juu ya Msikiti wa Pili
kwa ukubwa duniani “Masjid Sultan” ambayo Taa yake inayoonekana kwa juu
ina uzito wa Tani nane ikiwa imebeba Balbu 2220. Watanzania
Wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa na Utamaduni walienda
kutembelea Msikiti huo kujifunza zaidi.
Picha zote-Faki Mjaka-Mascut Oman
Wafanyakazi wa Msikiti wa Pili kwa
ukubwa duniani “Masjid Sultan” wakijibu maswali na kutoa ufafanuzi
kutoka kwa Watalii mara baada ya kumaliza kutembelea msikiti huo.
Watanzania Wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa na Utamaduni
nchini Oman nao walienda kutembelea Msikiti huo kujifunza zaidi.
Wageni na Baadhi ya Watanzania
Wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa na Utamaduni nchini Oman
wakiwa Sehemu ya mbele (Qibla) ya Msikiti wa Pili kwa ukubwa duniani
“Masjid Sultan”. Msikiti huo umefanywa kama Kivutio cha Watalii na
kujifunza.Watanzania hao walienda kutembelea Msikiti huo kujifunza
zaidi.
Sehemu ya nje ya Msikiti wa Pili
kwa ukubwa duniani “Masjid Sultan”. Msikiti huo umefanywa kama Kivutio
cha Watalii na kujifunza ambapo Watanzania Wanaoshiriki Maonesho ya
Kimataifa ya Sanaa na Utamaduni nchini Oman waliutembelea Msikiti huo
kujifunza zaidi.
…………………………………………………………………….
Faki Mjaka-Mascut Oman
Taasisi za Kidini nchini Tanzania
zimeshauriwa kujenga Nyumba za Ibada zitakazokuwa huru kwa Mtu yeyote
kuzitembelea na kujifunza ili kuzidisha upendo na mshikamano miongoni
mwa jamii.
Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza chuki na misimamo mikali ya kidini inayoweza kutokea miongoni mwa Jamii husika.
Ushauri huo umetolewa na
Watanzania wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa na Utamaduni
baada ya kutembelea Msikiti Mkubwa wa Sultan Qabus uliopo Mascut nchini
Omani.
Msikiti huo wa pili kwa Ukubwa
Duniani umefanywa kama kivutio cha Utalii na Uwekezaji ambapo Wenyeji na
Wageni kutoka Mataifa mbalimbali hupata nafasi ya kuutembelea na
kuuliza chochote kwa Wafanyakazi wake.
Watanzania hao wamesema kuna mengi
ya kujifunza baada ya kutembelea Msikiti huo ambayo yanaweza yakasaidia
sana iwapo yataigwa nchini Tanzania.
Mmoja ya Watanzania hao Fred Halla
amesema nchini Tanzania Nyumba za Ibada hugeuzwa kuwa sehemu ya kwenda
kufanya Maombi na kuondoka kwa Waumini wa dini husika jambo ambalo
haliwaunganishi vyema Watanzania.
Amesema umefika wakati kwa Taasisi
za Dini kuzifanya Nyumba za Ibada kama kimbilio la watu wa dini Tofauti
kwenda kujifunza utamaduni na dini kwa usahihi wake jambo ambalo
linaweza kuzidisha upendo zaidi.
“Kule kwetu ni Ajabu Muislamu
kwenda Kanisani au Mkristo kwenda Msikitini lakini Katika Msikiti huu
unaingia unapotaka na kuuliza chochote na unapata majibu..kwa hili
unakuta unapata ukweli wa dini husika kinyume na unavyosikia Mtaani”
Alisema Fred.
Amesema alikuwa anaamini kuwa
Waislam ndio ambao wanaruhusiwa kuingia Msikitini tu lakini amebaini
kuwa Msikitini anaweza kuingia Mtu yeyote na kuuliza chochote ilimradi
kafuata sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Utawala
Ubalozi wa Tanzania nchini Oman Abdallah Kilima amesema mfano wa Miskiti
kama huo wa Sultan Qabus unaweza ukatumika pia kama njia ya kupunguza
Misimamo Mikali na uelewa mbaya wa dini.
Amesema ni vyema pia Tanzania kuwe
na utamaduni unaoruhusu Nyumba za Ibada kuwa sehemu ambayo Muumini wa
Dini yeyote anaweza kwenda na kuuliza kwa uhuru kama ilivyokuwa kwa
Masjid Sultan.
“Kuna mambo mengi watu
wanaaminishwa kuwa Misikitini Kuna hili na lile au Kanisani kuna hivi na
vile lakini mtu anapopata fursa ya kwenda na kujionea na kuuliza
maswali anaondoka akiwa amepata majibu sahihi na kuridhika kama Sisi
tulivyopata nafasi hiyo” Alisema Kilima.
Msikiti huo wa pili kwa ukubwa
duniani ulijengwa kwa muda wa Miaka sita kutoka mwaka 1995 hadi 2001
ambapo miongoni mwa maajabu yake ni kuwa na Taa kubwa yenye uzito wa
Tani 8 na balbu 1220.
Aidha Msikiti huo wenye huduma
Tofauti ikiwemo kumbi za kufanyia mikutano,Kituo cha Taarifa, pia
unauwezo wa kuchukua Waumini 10,000 kwa wakati mmoja na Maegesho ya
Magari 4,000 kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment