Naibu Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango na Mkuu
wa Kongane ya Biashara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kiuchumi, Bw. Paul
Sangawe (Kushoto) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Himaya
Moja ya Forodha jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa Masuala ya Forodha
kutoka TRA, Bw. Stambuli Myovela (Kulia) akizungumza wakati wa Semina
ya Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) kwa watumishi wa
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Baadhi ya watumishi wataalamu
wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakifuatilia kwa umakini mawasilisho
kuhusu Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) katika semina
iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Naibu Katibu Mtendaji (Huduma
za Jamii na Masuala ya Idadi ya Watu), Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango,
Bibi Florence Mwanri (Kushoto) akichangia mada wakati wa Semina ya
Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) kwa watumishi wa Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango
Bw. Elykedo Ngonyani ambaye ni
Mchumi Mwandamizi (Sekta za Uzalishaji) akichangia mada wakati wa Semina
ya Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) kwa watumishi wa
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
………………………………………………….
Na Saidi Mkabakuli
Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imetoa semina juu ya Himaya Moja
ya Forodha (Single Customs Territory) kwa watumishi na viongozi
waandamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Akizungumza katika ufunguzi wa Semina hiyo, Naibu Katibu
Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango na Mkuu wa Kongane ya
Biashara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kiuchumi, Bw. Paul Sangawe
amesema kuwa semina hiyo ina lengo la kuhakikisha kuwa kuna uelewa wa
pamoja kuhusu utaratibu huo kwa watumishi wa umma na watanzania wote.
“Lengo la semina hii ni kupata ufahamu wa kutosha kuhusu mambo
mbalimbali yanayoendelea, ili kuweza kushauri Serikali ipasavyo katika
masuala mbalimbali ya kisera katika Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki,” alisema Bw. Sangawe.
Akiwasilisha mada juu ya Mfumo wa Himaya Moja ya Forodha kwa
watumishi, Mtaalamu wa Masuala ya Forodha, Bw. Stambuli Myovela alisema
kwamba mfumo huo unaainisha utaratibu wa Mzunguko Huru wa Biashara,
Usimamizi wa Mapato, na Mfumo wa Kisheria.
Bw. Myovela aliongeza kuwa kwa mujibu ya mfumo uliokubalika ni
kwa kila Nchi Wanachama zitakushanya mapato yake ya kodi. Aidha, kwa
bidhaa zinazopitia Nchi moja kuelekea katika Nchi nyingine wanachama
(Transit Goods), Nchi Wanachama zimekubaliana kuwa nchi husika bidhaa
zinapokwenda itakusanya mapato yake na kuifahamisha mamlaka ya forodha
mizigo ilipoingilia katika Jumuiya kwa ajili ya kuruhusu bidhaa
kuondoshwa.
Akieleza namna ya utendaji kazi wa mfumo huo, Bw. Myovela
aliongeza: “Baada ya kuthibitisha kuwa kodi imelipwa, mizigo
itasafirishwa kutoka kituo cha kwanza cha forodha chini ya usimamizi wa
Mamlaka ya Forodha kwenda nchi ambayo mizigo hiyo imekusudiwa kutumika
ndani ya Jumuiya. Mfumo maalum wa ufuatiliaji kielektroniki (Electronic
Cargo Tracking System) utatumika kuhakikisha mizigo inafika salama
katika nchi iliyokusudiwa katika Jumuiya.”
Mfumo wa Himaya Moja ya forodha uliridhiwa na Baraza la Mawaziri
la Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wake wa 28 ambapo kwa
pamoja Mawaziri hao waliridhia kuwa na Mpangokazi unaoainisha masuala ya
kutekeleza katika kipindi cha miezi sita ili kuwezesha kuanzishwa kwa
Himaya Moja ya Forodha ifikapo mweizi Juni, 2014.
No comments:
Post a Comment