Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu ya kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Fereji
…………………………………….
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu ya
kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Fereji amesema ukataji wa miti aina ya
mikoko husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kufanya maji ya
bahari kuingia katika maeneo ya kilimo na makaazi ya watu.
Hayo ameyaeleza katika ukumbi wa
Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati alipokuwa akijibu suala la
Mwakilishi Bikame Yussuf Khamis alietaka kujua mpango wa dharura wa
Serikali katika kuyanusuru mazingira ya bahari ili kuviokoa visiwa
vidogo.
Waziri Fereji amesema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiyana na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inatarajia kutekeleza mradi wa kujenga uwezo wa
kuhimili athari za mabadiliko ya tabia ya nchi katika maeneo ya ukanda
wa pwani ya Tanzania utakaohusisha maeneo ya Bagamoyo , Pangani , Rufiji
na Zanzibar.
Amesema eneo la Kisiwapanza ni miongoni mwa maeneo ya
Zanzibar yanayotegemewa kuwemo kwenye mradi huu na tayari wataalamu wa
mradi huo wamefika Zanzibar kwa ajili ya kuangalia maeneo ya mradi
ambayo ni Kisiwapanza , Tumbe na Ukele kwa Pemba na maeneo ya Kilimani
na Bwawani kwa Unguja. Hivi sasa wataalamu hao wako katika hatua ya
mataarisho na kufahamu upeo wa mradi kwenye maeneo husika ambapo
Zanzibar imekadiriwa kupata kiasi cha dola za marekeni 361,300 kwa ajili
ya mradi huo. Akijibu suala la nyongeza aliloulizwa na Mwakilishi wa
Jimbo la Chonga Abdullah Juma, Waziri Fereji amesema Ofisi pekee haiwezi
kudhibiti kina cha maji ya bahari kwani ni suala la maumbile, hivyo
wananchi wanapaswa waelimishwe athari za uharibifu wa mazingira ili
waweze kuachana na vitendo hivyo.Wakati huo huo Naibu Waziri wa Afya
Mahmoud Thabit Kombo amesema sera ya Serikali ya matibabu bure Zanzibar
bado ipo na inaendelea kufanya kazi, licha ya kwamba wananchi wamekuwa
wakichangia kwango kidogo cha huduma za afya.Akijibu suala la Mh Ali
Salum Haji (Jimbo la kwahani ) aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa
kuanzisha sera ya msamaha kwa baadhi ya makundi ya watu wakiwemo wazee
wenye umri mkubwa na watoto chini ya miaka mitano kupata matibabu bila
malipo kama zilivyo nchi nyengine jirani.
Naibu Waziri amesema Wizara ya
Afya inaandaa miongozo ya uchangiaji wa huduma za afya ambapo makundi
maalumu yameainishwa kupatiwa msamaha wa kuchangia huduma hizo.
Ameyataja makundi hayo ni watoto
wenye umri chini ya miaka 5 wazee wasiojiweza , walemavu wasiojiweza,
watu wenye maradhi sugu kama vile ukimwi, kifua kikuu na saratani, na
kwa wale wasiokuwa na uwezo bado wanaendelea kupata huduma za afya
kulingana na taratibu zilizowekwa .
No comments:
Post a Comment