Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed
Shein (wa tatu kulia) Rais Mstaafu wa Zanzibar Alhaj Dk.Amani Abeid
Karume (kulia) na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhaj Balozi Seif
Ali Iddi pamoja na Viongozi wengine na waislamu mbali mbali wakijumuika
kwa pamoja kumswalia aliyekuwa Mshauri wa Rais wa Utalii Marehemu Issa
Ahmed Othman katika Masjid Mahfoudh Mazizini, Marehemu alifariki juzi
Nchini India na kuzikwa leo Kianga Wilaya ya Magharibi Unguja,[Picha na
Ikulu.] Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed
Shein, (katikati)Rais Mstaafu wa Zanzibar Alhaj Dk.Amani Abeid Karume,
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhaj Balozi Seif Ali Iddi pamoja na
Viongozi mbali mbali na Waislamu mbali mbali wakijumuika kwa pamoja
kumuombea dua baada ya kumswalia aliyekuwa Mshauri wa Rais wa Utalii
Marehemu Issa Ahmed Othman katika Msikiti Masjid Mahfoudh
Mazizini,Marehemu amezikwa leo Kijiji cha Kianga Wilaya ya Magharibi
Unguja,[Picha na Ikulu.] Baadhi
ya Vijana na wananchi waliobeba Jeneza la Marehemu Issa Ahmed Othman
aliyekuwa Mashauri wa Rais Utalii Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
wakiupeleka kuzikwa kijijini Kianga Wilaya ya magharibi Unguja leo
jioni,marehemu alifariki juzi Nchini India ambako alikwenda kwa
matibabu,[Picha na Ikulu.]
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed
Shein na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhaj Balozi Seif Ali Iddi
(katikati) pamoja na Viongozi wengine na waislamu mbali mbali
wakijumuika kwa pamoja katika mazishi ya aliyekuwa Mshauri wa Rais wa
Utalii Marehemu Issa Ahmed Othman katika Kijiji cha Kianga Wilaya ya
Magharibi Unguja leo jioni,[Picha na Ikulu.]
……………………………………………………………………………………………..
Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar
Aliyekuwa Mshauri wa Rais wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mambo ya Utalii Mhe. Issa Ahmed
Othman amefariki dunia baaada ya kuugua kwa muda mrefu.
Marehemu Issa Ahmed alifariki siku
ya tarehe 25/01/2015 akiwa katika matibabu nchini India na amezikwa
jana katika kijiji cha Kianga nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ambapo kifo
chake kimeleta mshtuko, huzuni na masikitiko makubwa kwa Chama Cha
Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Marehemu alizaliwa mnamo tarehe 24
Julai, 1951 katika kijiji cha Pandani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini
Pemba na kupata elimu yake ya msingi katika Skuli ya Pandani Pemba na
baadae kupata elimu ya sekondari Uweleni Pemba na kufaulu kidato cha nne
pamoja na masomo ya Qur-aan aliyoyapata hapohapo kijijini kwao.
Katika jitihada za kupanua elimu
yake Marehemu alijiunga na Chuo cha Uhasibu na kufaulu kuwa mhitimu wa
Taaluma ya Uhasibu katika ngazi ya Stashahada.
Kwa upande wa utumishi Marehemu
alishika nyazifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
zikiwemo; Mkaguzi wa Ndani (1969-1974), Mhasibu Wizara ya Biashara Pemba
(1975-1984), Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (1985-1995), Naibu Waziri
wa Kilimo, Mifugo na Maliasili Zanzibar (1988-1995), Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima Zanzibar (1987-2000), Makamo
Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Bandari (1988-1999),
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar (2000-2010), Mshauri wa Rais
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mambo ya Utalii 2010 hadi mauti
yalipomfika.
Kwa upande wa chama, Marehemu
alikuwa ni Mwanachama wa Afro Shirazi Party (ASP) na baada ya kuungana
kwa vyama vya TANU na ASP mwaka 1977 akawa Mwanachama mwanzilishi wa
Chama Cha Mapinduzi.
Katika kuendeleza jitihada zake za
kisiasa na kupata ushirikiano mzuri na wanachama wenzake Marehemu
alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha
Mapinduzi nafasi ambayo ilimjengea umaarufu na kumuwezesha kushika
nafasi za juu za Uongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inatambua mchango mkubwa wa Marehemu Issa Ahmed
katika Utumishi na Uongozi wa Chama hicho katika maisha yake kwa kuwa
alikuwa ni Kiongozi mwenye Kuheshimu watu, Mchapakazi mahiri, Mweledi na
aliyekuwa akitegemewa na wengi nchini Zanzibar na bila ya shaka kifo
cha Marehemu kimeacha pengo kubwa katika Chama Cha Mapinduzi na Taifa
kwa ujumla.
Aidha Chama na Serikali vimewataka
Viongozi, Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Marehemu kuwa na moyo wa subira
katika wakati huu mgumu wa maombolezo ya mpendwa wao huyo.
Hadi kufariki kwake, Marehemu Issa
Ahmed Othman alikuwa ni mshauri wa Rais katika mambo ya Utalii
Zanzibar, na ameacha Kizuka 1, Watoto 7, na Wajukuu 25.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahala pema Peponi.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment