Tarehe
8 Machi, 2015 Tanzania itaungana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa
kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Kwa mwaka huu, tunaadhimisha siku
hii adhimu katika ngazi ya kitaifa ambapo mkoa wa Morogoro utakuwa
mwenyeji wa Maadhimisho haya. Mikoa mingine itakuwa na fursa ya kuandaa
maadhimisho haya katika maeneo yao kwa kuzingatia mazingira yao.
Maadhimisho haya hutoa fursa kwa
Taifa, mikoa, wilaya na wadau wengine kupima mafanikio yaliyopatikana
katika kuwendeleza wanawake na kubainisha changamoto zilizojitokea
katika kuwawezesha wanawake na kuweka mikakati ya kukabiliana na
changamoto hizo.
Maadhimisho ya mwaka 2015 ni ya
kipekee kutokana na kuwepo kwa matukio muhimu ambayo yote yatagusa
masuala ya haki za wanawake na usawa wa jinsia. Matukio hayo ni:
Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge, na madiwani; tathmini ya mafanikio ya
utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing baada ya miaka 20 (1995 –
2015); tathmini ya Malengo ya Millenia (2005-2015) na mwelekeo wa Agenda
2063; kuhusu kuwa na ‘Afrika Tunayohitaji’ ifikapo mwaka 2063.
Kufuatia umuhimu huu Wizara
imeandaa Kongamano la Kitaifa litakalofanyika tarehe 6 Machi, 2015 na
maonesho ya shughuli mbalimbali sanjari na utoaji wa tuzo kwa
waliochangia uwezeshaji wa wanawake nchini.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani mwaka 2015 ni: ‘Uwezeshaji Wanawake; Tekeleza Wakati
ni Sasa’. Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha jamii kutambua mchango wa
wanawake katika kuleta maendeleo yao; na kuelimisha wadau kuangalia upya
wajibu wao wa kuwashirikisha, kuwaamini na kuwapa wanawake haki sawa
katika nafasi za elimu, uchumi na uongozi ili waweze kuwa chachu katika
maendeleo yao.
Natoa wito kwa wananchi katika
mikoa yote nchini kushiriki kikamilifu kuienzi siku hii adhimu. Ni
matumaini yangu kwamba kupitia maadhimisho haya wadau wote na serikali
watakumbushwa wajibu na mchango wao katika kutekeleza ujumbe wa
kaulimbiu na kubaini mbinu za kukabiliana na changamoto za ushiriki wa
wanawake katika maendeleo.
Aidha, nawaomba wanahabari
kushirikiana na Serikali kuelimisha jamii kuhusu shuhuda bora
zinazoonyesha jinsi gani wanawake walivyoweza kuaminiwa na hivyo kutoa
mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Nawatakia maadhimisho mema.
Anna T. Maembe
KATIBU MKUU
19/03/2015
No comments:
Post a Comment