Mahmoud Ahmad -Arusha
Mahakama kuu ya Tanzania
imepokea msaada wa mashine 38 za kupiga chapa Kutoka Mahakama ya mauaji
ya Kimbari(ICTR) itakayorahisisha upatikanaji wa nakala za hukumu na
mwenendo wa kesi mbalimbali hapa nchini.
Akipokea Msaada huo Jaji Mkuu wa
Tanzania Mohammed Chande Othman alisema kuwa msaada huo utasaidia
upatikanaji wa haki kuwa rahisi pia, kwani umekuja wakati muafaka wakati
mahakama ikiwa katika mabadiliko ya kuzifanya kesi kwenda kwa wakati.
Jaji Othman alisema changamoto
ya utoaji haki kwa wakati imeweza kurahisishwa kwa upatikanaji wa
mashine hizo ambazo ni za kisasa na za gharama ambazo zimeipunguzia
mzigo serikali.
“Mashine hizi za msaada baada
ya kupatikana sasa ni mwendelezo wa mashirikiano yetu kati ya serikali
na mahakama hii ikiwemo ukamataji wa wahalifu, kuwatunza na kuwalinda
hivyo ni moja ya faida za mashirikiano hayo”alisema Jaji Mkuu.
Alisema kuwa ushirikiano uliopo
kati ya mahakama ya kimataifa ya mauaji ya kimbari na serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wa muda mrefu kuanzia kwenye
ukamataji wa wahalifu wa mauji hadi kuwahifadhi hivyo hii sehemu ya
mashirikiano hayo ya muda mrefu.
Jaji Othman alisema kuwa Hatua
ya msaada huo itaendana vizuri na ufundishaji wa makatibu wetu ilikuweza
kufanyakazi kiufanisi kwa kutumia msaada huo wa vitendea kazi hivyo
akaiomba mahakama hiyo kuendana na mbio za kiutendaji ili kufanikisha
upatikanaji haki kwa wakati.
Mashine hizo zenye thamani ya
dolla 95,000 zimetolewa na mahakama ya mauaji ya Kimbari kwa mahakama
yetu ili ziwezekusaidia kupunguza malalamiko na uchelewaji wa kutoa
nakala za hukumu na mwenendo wa kesi za jinai hapa nchini.
“Vitendeakazi hivi vimekuja
wakati muafaka kwani tumekuwa katika mikakati ya ubadilishaji wa
utumiaji wa kuandikia mikono kwenda kwenye utumiaji wa vifaa
kutakakorahisisha kutoa hukumu na mwenendo wa kesi kwa wakati na kuacha
kutumia muda mrefu kupata nakala za hukumu na mwenendo wa kesi
mbalimbali” alisema Jaji Othman.
No comments:
Post a Comment