Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania linapenda kutoa taarifa ya kifo cha Askari wake Praiveti Ahadi
Mwaka Mwainyokole kilichotokea tarehe 4 Februari 2015 katika mji mdogo
wa Mbalizi, Mkoani Mbeya.
Taarifa za mazingira ya kifo cha
Askari huyo zimepotoshwa na baadhi ya Vyombo vya Habari na kusababisha
mapokeo tofauti kwa wananchi.
Hali halisi ni kwamba, mnamo
tarehe 4 Februari 2015 Askari huyo akiwa na Askari wenzake wanne (4)
ambao ni Koplo Bedatu Benard Mloka, Praiveti Thani Hamisi Haji, Praiveti
Mzee Buan Mzee na Praiveti Mohamed Juma walivamiwa na kundi la wahuni
wakati wakitoka matembezini. Chanzo cha vurugu hizo ni kutokana na
Praiveti Rashid Maulid wa Kikosi chao kuibiwa samani kwenye nyumba
aliyokuwa amepanga uraiani katika mji mdogo wa Mbalizi, Kitongoji cha
Shigamba. Samani alizoibiwa ni pamoja na TV aina ya LG “flat screen”
“Inch 20”, radio aina ya Sony moja, Deck aina ya Sangsung, flash moja,
extension cable moja na fedha taslimu Tshs 30,000/=.
Askari huyo alitoa taarifa Kituo
cha Polisi tarehe 03 Februari 2015 na kupatiwa RB yenye Nambari
MBI/RB/285/2015, sambamba na kutoa taarifa Polisi. Kituo hicho cha
Polisi kilitoa askari mmoja ambae aliungana na askari Jeshi na wenzake
na wakaenda eneo la relini ambako vijana wasio na ajira maalumu
hushinda. Waliwakamata vijana saba, mmoja wa vijana hao alikimbia na
kwenda kuwapa taarifa wenzao ambao hawakuwepo katika eneo hilo ambapo
vijana sita walifikishwa kituo cha Polisi.
Ilipofika saa tatu usiku askari
hao wakiwa katika matembezi ya kawaida walikutana na kundi la vijana
wakiwa na silaha mbalimbali kama nondo na marungu ambao walianza kuwa
shambulia huku wakiwashutumu kuwa waliwapeleka wenzao Polisi.
Kwa kuwa kundi la vijana hao
lilikuwa kubwa na likiwa na silaha zilizotajwa lilifanikiwa kuwajeruhi,
Askari hao akiwemo Praiveti Ahadi Mwainyokole ambae alijeruhiwa
vibaya. Askari hao walikwenda Polisi na wakachukuwa PF3 na kisha kwenda
katika hospitali ya Jeshi Mbeya baadaye Praiveti Mwainyokole alifariki
muda mfupi baada ya hali yake kutokuwa nzuri kutokana na kupigwa na kitu
kizito kichwani hali iliyosababisha damu kuvia kwenye Ubongo.
JWTZ linasikitishwa na mauaji
hayo yaliyofanywa kwa Askari wake, na mauaji ya askari wengine katika
maeneo ambako vitendo kama hivyo vimetokea. Ikumbukwe kuwa JWTZ lipo kwa
ajili ya usalama na ustawi wa wananchi, hivyo JWTZ linalaani vitendo
viovu vinavyofanyika kwa askari wake na linatoa rai kwa vyombo vya
sheria kuchukua mkondo wake.
Kimsingi JWTZ halina ugomvi na
wananchi kwani kazi yake ya msingi ni kuwalinda ili waweze kutekeleza
majukumu yao ya kimaendeleo kwa utulivu na amani kwa ajili ya ustawi wa
Taifa letu.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
No comments:
Post a Comment