Nchini
Tanzania kumetokea mkasa mwingine kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi,
albino kutekwa katika wilaya ya Chato mkoa wa Geita, kaskazini magharibi
mwa nchi hiyo.
Polisi wameeleza kuwa mtoto huyo aliyetajwa kwa
jina la Yohana Bahati mwenye umri wa mwaka mmoja alitekwa nyumbani kwao
na watu wasiojulikana jana usiku.
Kwa mujibu wa taarifa za
mwandishi kutoka eneo hilo Renatus Masuguliko, polisi wamefika eneo la
tukio na kuanza msako mkali dhidi ya watu wanaotuhumiwa kufanya kitendo
hicho.
Habari zinasema watu waliokuwa na silaha za jadi waliwaweka
chini ya ulinzi Bahati Misalaba na mkewe ambao ni wazazi wa mtoto
albino ambaye walimteka na kutoweka naye.
Familia hii pia ina
watoto wengine wawili wenye ulemavu wa ngozi, Tabu Bahati mwenye umri wa
miaka miwili na Shida Bahati mwenye miaka kumi na mmoja ambao
walinusurika kuchukuliwa na watu hao kwa sababu wakati unyama huo
ukitendeka nyumbani kwao hawakuwepo walikwenda kucheza kwa majirani zao.
Mama wa mtoto huyo alijeruhiwa vibaya wakati akimpigania mtoto wake asichukuliwe na watu hao.
No comments:
Post a Comment