Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na mauaji ya
kikatili ya mtoto Yohana Bahati aliyetekwa nyara hivi karibuni katika
kijiji cha Ilelema, Chato Mkoani Geita.
Pia Tume inalaani kuumizwa kwa
mama yake, Ester Jonas wakati anatetea uhai wa mwanae wakati wa tukio
lililotokea Februari 15, 2015.
Tume inapenda kuwakumbusha
wananchi kwa ujumla kuwa vitendo vya ukatili wanaofanyiwa watu wenye
ulemavu wa ngozi, ni matukio ya ukiukwaji wa Sheria na haki za
kibinadamu. Matukio haya yanaonesha yamekuwa yakichagizwa na imani za
kishirikina hivyo Tume inakemea matendo haya na kutaka yapigwe vita.
Chini ya Katiba na Mikataba ya
Kimataifa ya Haki za Binadamu Serikali inao wajibu wa kulinda raia wake.
Tume inaiomba Serikali kuwatafuta wale wote wanaohusika na vitendo hivi
na kuwafikisha mbele ya vyombo vya Sheria.
Aidha, Tume inaungana na wananchi,
wadau mbalimbali na Serikali kulaani vikali mauaji ya mtoto Yohana
Bahati na kujeruhiwa vibaya mama yake wakati akitetea haki ya mwanae
kuishi katika jamii huru, na inakemea vikali vitendo hivyo vya kikatili
dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa ujumla.
Tume inaikumbusha Serikali kuwa
wakati umefika wa kufanyia marekebisho makubwa Sheria ya Uchawi (Sura ya
18 ya 1928) au kutunga Sheria mpya ili kupiga marufuku vitendo vyote
vinavyoendeleza imani za uchawi na ushirikina.
Tume inashauri pia Serikali kupitia upya Sheria inayowatambua waganga wa jadi (Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala).
Tume inatoa wito kwa wananchi na
jamii yote kwa ujumla kuachana na imani potofu zenye mtizamo hasi kwamba
mafanikio yoyote yanaweza kupatikana kwa njia za kishirikina. Tume
inakumbusha wananchi kuwa mafanikio yoyote yatapatikana kwa kufanya kazi
zote halali kwa bidii, na siyo kwa njia za kishirikina ikiwemo kutumia
viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Tume inaungana na wananchi na Serikali kupiga vita vitendo hivi vya kikatili.
Pia Tume inatoa pole kwa mama aliyeumizwa akitetea uhai wa marehemu mwanae.
Mwisho Tume iko mbioni kwa
kushirikiana na wadau wengine kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuelimisha
wananchi ili kuepusha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
Tume inaomba wananchi wote kushirikiana katika jukumu hili.
Imetolewa na:
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Februari 19, 2015
No comments:
Post a Comment