Na Anna Nkinda – Maelezo
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) na Serikali ya Japani wametiliana saini mkataba wa mradi wa
upanuzi wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Rufiji mkoani
Pwani utakaogharimu shilingi milioni mia tisa.
Utiaji saini wa mkataba huo
umefanyika leo katika ofisi za WAMA zilizopo jijini Dar es Salaama kati
ya Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Mama Salma Kikwete na Balozi wa Japani
nchini Masaki Okada.
Akiongea mara baada ya kusaini
makubaliano hayo Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete aliishukuru Serikali ya Japani kwa kuwajali watanzania na
kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha elimu.
Alisema mradi huo utapanua na
kuboresha uwezo wa shule kutoa huduma bora ya elimu ambapo kutakuwa na
upanuzi wa jengo la utawala kwa kuongeza ghorofa moja ili kupata chumba
cha walimu ambao wataweza kufanya mikutano yao, kituo cha walimu, na
maktaba.
Ujenzi wa chumba maalum cha
kompyuta ambacho kitawafanya wanafunzi kusoma somo hilo kwa vitendo,
uwekaji wa mitambo ya mawasiliano kwa ajili mtandao wa Internet katika
eneo la shule ambao haukuwepo shuleni hapo.
“Pia ninawashukuru kwa msaada wa
vitabu vya kiada na ziada ambavyo vitafika hivi karibuni , elimu ni
kitabu na ukisoma bila kitabu hutakuwa na mapana zaidi, tukipata vitabu
vya ziada vitasaidia kujenga ufahamu wa mtoto kuweza kuchanganua mambo
mbalimbali”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Balozi Okada
alisema mradi huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni ujenzi
wa maabara ya kompyuta pamoja na kutoa vifaa muhimu na kuunganisha
Broadband Internet kwenye maabara.
Balozi Okada alisema, “Baada ya
mradi huu kukamilika sio tu wanafunzi wataweza kujifunza kompyuta bali
pia watatumia internet kupata taarifa nyingi na za kisasa zinazopatikana
mtandaoni.
“Sehemu ya pili ni upanuzi wa
jengo la utawala. Mradi huu ukikamilika wanafunzi hawatapata tabu ya
kutafuta walimu kwa ajili ya kuuliza maswali kuhusu masomo. Ninaamini
kwamba mazingira bora kwa walimu yanaboresha mazingira ya kusomea kwa
wanafunzi”.
Aidha Balozi Okada alisema Hayao
Nakayama ambaye ni mtu wa kwanza kutoa ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa
shule hiyo ametoa zaidi ya milioni mia moja na themanini ambazo
zitatumika kwa ajili ya kununulia gari la dharura la kubebea wagonjwa
na maelfu ya vitabu ambavyo vitasafirishwa siku za karibuni kutoka
nchini Japani.
Balozi huyo alisema vitabu hivyo
siyo tu vya masomo ya sayansi na hisabati vinavyohitajika kuongeza
ujuzi lakini pia kuna vitabu vya kiingereza na kiswahili kama vile
hadithi, riwaya halisi pamoja na wasifu wa watu mashuhuri wanaume na
wanawake kutoka duniani kote ikiwamo Japani.
“Wanafunzi watajifunza hadithi za
mashujaa waliopigania elimu kwa wanawake na waasisi wa kampuni kubwa
kama vile Panasonic na Honda. Wataweza kupata watu wa mfano wa kuigwa
kati ya hao wataweza kujifunza kutokana na maisha yao jinsi
walivyotekeleza ndoto zao na kuishi siyo tu kwa ajili yao binafsi bali
kwa familia, marafiki na watu katika jamii na taifa kwa ujumla”, Balozi
Okada alisema.
Shule ya Sekondari ya
WAMA-Nakayama yenye wanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza hadi cha tano
wengi wao wakiwa ni watoto yatima na wanaoishi katika mazingira
hatarishi ilianza mwaka 2010 ikiwa na wanafunzi 83 na hadi sasa ina
wanafunzi 366.
No comments:
Post a Comment