WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wasikilize na kufuata
mafundisho yanayotolewa na viongozi wa dini ili Tanzania iwe nchi
yenye watu waadilifu na wenye hofu ya Mungu.
Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Februari 20, 2015) wakati
akizungumza na maelfu ya waumini na wananchi waliohudhuria ibada ya
mazishi ya Askofu Mstaafu Magnus Mwalunyungu kwenye kanisa la Moyo
Mtakatifu wa Yesu la Tosamaganga, Jimbo Katoliki la Iringa.
“Leo ni siku ya pekee ya kuwasikiliza viongozi wa dini wakituasa
tujiandae kwa maisha baada ya kifo. Tukio hili la leo litupe nguvu ya kukubali kwamba kifo kipo licha ya kuwa hakizoeleki na kinapotokea kinaleta simanzi kubwa,” alisema.
“Ninawasihi Watanzania wote tufuate mafundisho yanayotolewa na
viongozi wa dini zetu ili Tanzania iwe na kundi la watu wenye hofu ya
Mungu, waadilifu na wanyofu kama ambavyo mahubiri ya leo
yamesisisitiza,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku tano ya kikazi mkoani
Iringa, aliamua kusitisha ziara yake siku ya leo ili aweze kushiriki
msiba huo. Pia alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Jakaya
Kikwete ambaye yuko Kenya kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Akitoa mahubiri kwenye ibada hiyo, Askofu Damian Dallu wa Jimbo Kuu
Katoliki la Songea alisema wanadamu wanahangaika na kuogopa kifo kwa
sababu hawajui baada ya kifo maisha yao yatakuwaje.
“Askofu Mwalunyungu ameishi kwa miaka 85 na kati ya hiyo, miaka 55
alikuwa akitumikia kama padre na kwa miaka 22 alimtumikia Mungu aakiwa
Askofu. Na hata baada ya kustaafu aliomba awe Parokopale Kidamalai
ambako alitumikia kwa miaka minne. Maisha yake yanaendana na neno
kutoka kitabu cha hekima kwamba kifo cha mwadilifu ni kupumzika kwa
starehe,” alisema.
Ibada hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na Maaskofu wa kanisa katoliki zaidi ya 20.
No comments:
Post a Comment