Taasisi
ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo Endelevu (UONGOZI Institute)
imeandaa mkutano wa kikanda utakaokutanisha viongozi na watunga sera
kutoka nchi za Afrika mashariki kuzungumzia changamoto za ukuaji wa
miji na kushughulikia hali ya baadaye ya miji ya Afrika.
Mkutano
huu uliopewa jina la, ‘Maisha ya baadae ya nchi za Afrika Mashariki:
Jinsi gani tunataka kuishi mwaka 2050’, utafanyika katika hoteli ya
Hyatt Regency Dar es Salaam, Kilimanjaro Hotel tarehe 19 na 20 Februari
ambapo Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Mizengo Pinda (Mb), atakuwa mgeni
rasmi.
Afisa
Mtendaji Mkuu wa UONGOZI Institute, Prof. Joseph Semboja alisema kwamba
jukwaa hilo linalenga kuangalia na kujadili changamoto na fursa
mbalimbali zinazoletwa na ukuaji wa miji Afrika Mashariki na jinsi gani
viongozi wa Afrika wanaweza kukabiliana nazo kwa pamoja.
“Kuna
uwiano mkubwa wa ongezeko la watu Afrika (na duniani kwa ujumla)
wanaoishi mijini na kupelekea msongamano na shinikizo la nyumba, ajira
na huduma za kijamii. Ni kwa matokeo haya jukwaa hili limelenga kujadili
namna ya kutatua changamoto hizo na kufikiria miji ambayo itatimiza
matakwa yetu,” alisema Prof. Semboja.
Kwa
mujibu wa chapisho la UN-Habitat ‘Hali ya miji ya Afrika 2014’ ,
“Afrika Mashariki inashika nafasi ya chini katika miji inayokua duniani
lakini ndiyo kanda inayoongoza katika kasi ya ukuaji wa miji yake hivi
sasa. Ifikapo mwishoni mwa muongo huu wa sasa idadi ya wakazi waishio
mijini itaongezeka kwa asilimia 50 na jumla ya idadi ya wakazi wa mijini
ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa kuwa mara tano ya 2010.
Hivyo
basi, ukanda wa Afrika Mashariki utakumbwa na changamoto zitakazotokana
na ongezeko kubwa la idadi ya watu mijini; ongezeko kubwa la madai
mapya na ya ziada kwa ajili ya utoaji wa nyumba za kutosha na kwa
gharama nafuu na huduma mijini, na pengine muhimu zaidi, fursa ya
kuzalisha kipato mijini.”
“Ni
dhahiri kwamba ukuaji wa miji na maendeleo mijini ni matokeo chanya ya
maendeleo ya binadamu na ukuaji wa kiuchumi kama tunaweza kuyakabili
kiusahihi. Na hii ndiyo maana nzima ya mkutano huu…Kutuweka katika njia
sahihi kwa kutambua vipaumbele vya juu na vitu muhimu kwa ajili ya
maendeleo," aliongeza Prof. Semboja.
Washiriki
wa kongamano hili watatoka: Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia,
Sudan ya Kusini, Tanzania na Uganda. Waalikwa watakuwa wawakilishi wa
ngazi za juu kutoka serikalini, mashirika ya kikanda na kimataifa, miji
mikubwa, wasomi, sekta binafsi na asasi za kiraia.
No comments:
Post a Comment