Abiria wakishuka toka kwenye ndege mpya ya Shirika la Ndege la Taifa,
Air Tanzania (ATCL) aina ya CRJ-100 yenye uwezo wa kubeba abiria 50
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki wakitoa mkoani Kigoma. Huo ukiwa ni mkakati wa
kimaendeleo wa shirika hilo katika kuongeza idadi ya ndege na safari
zake. Picha na mpiga picha wetu.
Meneja wa Air Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, Bw James Mbago akizungumza na waandishi wakati wa
uzinduzi wa ndege mpya ya shirika hilo aina ya CRJ-100 yenye uwezo wa
kubeba abiria 50, mara baada ya ndege hiyo kutua ikitokea mkoani Kigoma.
Huo ukiwa ni mkakati wa kimaendeleo wa shirika hilo katika kuongeza
idadi ya ndege na safari zake
SHIRIKA la ndege la Taifa (ATCL) mwishoni mwa wiki
iliyopita lilizindua ndege yake mpya aina ya CRJ-100 yenye uwezo wa
kubeba abiria 50 ikiwa ni sehemu ya mpango wa shirika hilo kuongeza
idadi ya ndege zake sambamba na kuongeza idadi ya safari zake.
Shirika hilo ambalo kwa sasa linalotoa huduma zake katika
mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Mtwara na visiwa vya Komoro limejipanga
kufanya safari za kila siku kati ya mikoa ya Dar es Salaam na Kigoma
huku pia likiwa tayari kufanya safari za Mtwara na visiwa vya Komoro
mara sita kwa wiki katika siku za Jumatatu, Alhamisi na Jumamosi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
mara tu baada ya ndege hiyo kutua kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), Meneja wa shirika hilo katika kiwanja hicho,
James Mbago alisema ndege hiyo imekodiwa kutoka nchini Afrika Kusini kwa
jitihada za Serikali ya Tanzania na sasa ipo tayari kuwahudumia wateja
wa shirika hilo.
“Kuja kwa ndege hii kunaongeza idadi ya ndege zetu hadi
kufikia mbili na tunashukuru kuona kwamba imepokelewa vizuri na abiria
wetu. Ndege yetu nyingine aina ya De-Havilland Dash 8 Q300 kwa sasa
inapata matengenezo makubwa kwenye karakana yetu iliyopo hapa hapa
uwanja wa ndege,’’ alisema Mbago.
Kwa mujibu wa Mbago kupona kwa ndege hiyo inayofanyiwa
matengenezo kiwanjani hapo kutalifanya shirika hilo lianzishe tena
safari zake za ndani kwa mikoa ya Mwanza, Tabora, Arusha na Mbeya.
“Muda si mrefu mambo yatakuwa mazuri zaidi…inafurahisha
zaidi tunapopata mrejesho mzuri kutoka kwa wateja wetu wanaofurahia
huduma za shirika lao mama,’’ aliongeza Mbago. Zaidi, Mbago aliongeza kuwa shirika lake linatarajia
ongezeko kubwa la abiria kutokana na ukweli kuwa ndege yao hiyo mpya ina
uwezo wa kusafiri kwa haraka zaidi ikilinganishwa na ndege nyingine
huku safari zake zikiambatana na huduma nzuri inayotolewa kwa wateja
wake.
Wakizungumza mara tu baada ya kushuka kwenye ndege hiyo,
baadhi ya abiria waliotoka Kigoma walisema licha ya kutumia muda mfupi
zaidi lakini pia walifurahia huduma nzuri walizozipata kutoka kwa
wahudumu wa ndege hiyo.
“Kwa kweli hii ilikuwa ni moja ya safari zangu za ndege
ambayo nimeifurahia sana. ATCL wanahitaji pongezi kwenye hili na zaidi
wafikirie kuboresha huduma zaidi ya hapa…sisi abiria tupo tayari
kuwaunga mkono kwa sababu ndio wanabeba nembo ya taifa letu,’’ alisema
mmoja wa abiria hao aliyejitambulisha kwa majina Gaudence Kashoka.
No comments:
Post a Comment