NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TAHARUKI iliyosambaa jana kwenye mitandao kijamii juu ya kuuzwa
kwa Clouds Media Group, inayomiliki Clouds FM, Clouds Tv na Choice FM,
zimepata majibu baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Joseph
Kusaga, kuibuka na kukataa habari hizo na kuziita ni uzushi wa kupuuzwa.
Habari za kuuzwa kwa kampuni hiyo
dhidi ya mfanyabiashara maarufu na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
Rostam Aziz, zilishika nafasi katika mitandao ya kijamii na hatimae
kuzua usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi, viongozi wa Clouds na Watanzania
kwa ujumla.
Akizungumza leo asubuhi (jana)
moja kwa moja katika kituo cha Radio cha Clouds FM, Kusaga alisema
habari hiyo imetengenezwa na watu walioamua kupoteza muda wao katika
mitandao ya kijamii, hali ya kuwa wapo wanaovuna fedha nyingi kwa
kupitia njia hiyo ya mawasiliano (social media).
Alisema mara baada ya kuenea kwa
habari hiyo, usumbufu mkubwa uliibuka kutokana na watu wenye mapenzi
mema na kampuni hiyo kuanza kuhoji juu ya taarifa hizo kama zina ukweli,
huku akisisitiza pia si kosa kuuza kwa kuwa ni jambo la kawaida katika
mambo ya kibiashara.
“Clouds Media Group ni kampuni
iliyoanzia chini kwa ushirikiano wa watu wengi, hivyo kuamua kuiuza
kiholela ni jambo la kushangaza, ingawa pia si dhambi kufanya hivyo kwa
mtu yoyote kwa sababu ni biashara kama zilivyokuwa biashara nyinginge.
“Naomba Watanzania wote wapuuze
habari hizo na kuwataka wale wenzetu walioamua kuitumia mitandao vibaya
waache na badala yake wajikite kufanya biashara kwa kupitia mitandao
hiyo ambayo inalipa kama itatumiwa vizuri na si kueneza habari za
kumuuzia Rostam ukizingatia kuwa hakuna kitu kama hicho na nina miaka
sijakutana na mfanyabiashara huyo katika kikao chochote cha kujadili juu
ya jambo hilo,” alisema Kusaga.
Aidha Kusaga alitumia muda huo
kuwahakikishia Watanzania kuwa Clouds ni chombo huru kisichofungamana na
chama chochote cha siasa, huku akisema kwamba katika Uchaguzi Mkuu
mwaka huu haki itatolewa kwa vyama vyote na wanasiasa wote.
“Huu ni mwaka mgumu, hivyo naomba
niseme ikitokea suala la kuhoji au kuunga mkono siasa, basi haki
itatolewa kwa wanasiasa wote, ukizingatia kwamba chombo chetu hakika
chama cha siasa inachokiunga mkono kwa sababu zozote zile,” alisema
Kusaga .
Katika hatua nyingine, Kusaga
aliwataka Watanzania wote kuunga mkono juhudi za kupambana na dawa za
kulevya, huku akisema sakata hilo linaathiri nguvu kazi ya Taifa,
hususan kwa baadhi ya wasanii waliojiinga katika matumizi hayo ya dawa
za kulevya.
“Sisi Clouds tunaungana na
Watanzania wote wanaopambana juu ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya,
hivyo ni jukumu letu kubwa kuzidi kuelimisha jamii juu ya masuala hayo
kwakuwa yanaathiri kwa kiasi kikubwa ndugu zetu, wakiwamo baadhi ya
wasanii,” alisema.
Kwa mujibu wa Kusaga, jitihada
nyingi zinawekwa katika kubuni mbinu mbalimbali za kuelimisha jamii
katika mambo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba Tanzania inapiga hatua
hatua katika nyanja za kielimu, kisiasa, kiuchumi na kijamii, huku
akiwataka watu kufanya kazi bila kuchoka na si kupoteza muda kwa kueneza
habari zisizokuwa na ukweli katika mitanda ya kijamii.
Clouds Media Group inayomiliki
kituo cha Radio cha Clouds FM, Clouds Tv na Choice FM, ni moja ya
makampuni ya wazawa yenye mafanikio makubwa, huku Watanzania wengi
wakifuatilia matangazo katika vituo hivyo
No comments:
Post a Comment