WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Iringa utafute njia bora
ya kuwasaidia wakulima wanaotumia na skimu ya umwagiliaji ya Magozi
katika tarafa ya Pawaga, wilayani Iringa ili waweze kunufaika na
matumizi ya zana za kisasa kwenye kilimo cha mpunga.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Iringa, Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo na uongozi wa vijiji hivyo, mara
baada ya kukagua eneo zima la mradi huo pamoja na zana za kilimo
walizonazo leo mchana (Alhamisi, Februari 19, 2015), Waziri Mkuu alisema
kwa zana walizonazo hawawezi kufikia lengo lao la uzalishaji wa tani
nane kwa ekari moja kama wataendelea na kilimo cha majaruba.
“Hii combine harvester
umesema inavuna ekari 12 kwa siku moja, sasa hapa kuna mtu ana robo eka,
jirani yake ana nusu eka, pale kuna mwingine ana ekari mbili utawezaje
kutumia mashine hii? Kimsingi haiwezekani,” alihoji Waziri Mkuu.
Alimtaka Mkuu wa Mkoa huo, Bi.
Amina Masenza awasiliane na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kupata taarifa
wao walifanyaje katika mradi unaohusisha wakulima wadogo na mwekezaji
kwenye kilimo cha mpunga wilayani Kilombero.
“Pangeni naye muone jinsi ya
kuwachukua baadhi ya wakulima wadogo wa kata hii ili waende huko na
kuona wenzao wamefanyaje kwenye kilimo kama chao lakini kinachotumia
zana za kilimo za kisasa,” alisema Waziri Mkuu.
“Kikubwa hapa ni kuwaunganisha wawe na ushirika, walime kwa staili ya block farm…
lakini wakishavuna kila mmoja apate mgao wake kulingana na eneo lake
analomiliki. Mkifanya hivi mtaona tija katika matumizi ya mashine hizi,
matumizi ya dawa za kuua magugu na hata matumizi ya mbegu bora,”
aliongeza.
Katika skimu hiyo ya umwagiliaji
ya Magozi, Waziri Mkuu alikagua mashine ya kupandia mpunga yenye uwezo
wa kupanda miche 1,856 kwa ekari moja ama ekari tano kwa siku moja. Pia
alikagua mashine ya kupurura mpunga yenye uwezo wa kupurura tani moja
nusu za mpunga kwa siku. Vilevile, alionyeshwa mashine mbili za kuvuna
mpunga ambapo kila moja ina uwezo wa kuvuna ekari 12.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili
mkoani Iringa jana jioni (Jumatano) akitokea Dodoma, ameanza ziara ya
kikazi ya siku tano katika mkoa huu ili kukagua shughuli za maendeleo.
No comments:
Post a Comment