Na Anna Nkinda – aliyekuwa Lindi
Wananchi wa mkoa wa Lindi
wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuipigia kura ya ndiyo katiba
inayopendekezwa kwani ni bora na imegusa maeneo yote kwa ajili ya
maendeleo ya Watanzania.
Rai hiyo imetolewa na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia
wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi
waliohudhuria sherehe ya kushangilia ushindi wa uchaguzi wa Serikali za
mitaa katika mtaa wa Ruaha kata ya Mingoyo wilayani humo.
Katika uchaguzi wa Serikali za
mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana wananchi
wa mtaa wa Ruaha waliwachagua Mwenyekiti na wajumbe wote watano kutoka
Chama Cha Mapinduzi.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema katiba inayopendekezwa imeangalia
maeneo yote yanayomgusa binadamu ikiwa ni pamoja na haki za wanawake na
watoto, watu wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu na wazee.
“Katiba iliyopo sasa ilitungwa na
baadhi ya watu waliokuwa madarakani kwa wakati ule na haikuwahusisha
wananchi, lakini hii inayopendekezwa wananchi wameshiriki kuitunga kwa
kutoa maoni yao”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Lindi Mwantumu Mahiza aliwahimiza wananchi hao kujiandikisha katika
daftari la kudumu la wapiga kura ili wasipoteze haki yao ya msingi ya
kupiga kura.
Mahiza alisema kama kuna watu
waliojiandikisha katika miaka ya nyuma wabebe vitambulisho vyao ili
viweze kunukuliwa na kwa wale wenye umri wa kuanzia miaka 18
wakajiandikishe na walio na umri wa chini ya hapo wasijiandikishe.
Aliwaasa wananchi hao kutokubali wageni waliokaa katika maeneo yao kwa kipindi cha chini ya miezi sita kujiandikisha.
Akisoma taarifa ya CCM tawi la
Ruaha Mohamedi Ngashona ambaye ni mjumbe alisema viongozi hao
wamejipanga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa mtaa huo
ambazo ni uharakishaji wa ujenzi wa zahanati, ukarabati wa vyumba vya
madarasa na ujenzi wa nyumba za walimu.
Kuwatambua kaya maskini na wazee
kwa kuwapatia huduma muhimu, uimarishaji wa barabara ya kutoka
Mnazimmoja hadi Ruaha na utekelezaji wa sera ya umeme vijijini hasa
vilivyopitiwa na mradi wa bomba la gesi.
Katika mkutano huo jumla ya wanachama 43 walijiunga na chama hiyo kati yao wanne walitoka Chama cha Wananchi CUF .
No comments:
Post a Comment