Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar. Ali Khalid Mirza akiwasilisha
Hotuba yake kwa mgeni rasmi Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi Sinnika
Antilla (Kulia) katika Uzinduzi wa Mfumo wa Mtandao wa Upatikanaji
Taarifa za Ardhi Zanzibar unaojulikana kama (Zanzibar Land Information
Service) (ZALIS) uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Ardhi iliyoko
Forodhani Mjini Zanzibar.
Kulia ni mgeni rasmi wa
Uzinduzi huo Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi Sinnika Antilla
akiwasilisha hotuba yake kwa katibu mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati (Kushoto) wakati wa uzinduzi huo.
Mgeni rasmi katika Uzinduzi huo
Balozi Antilla akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mfumo wa
Mtandao wa Upatikanaji Taarifa za Ardhi Zanzibar.
Wa Tatu (Kulia) ni Meneja wa mradi
wa ZALIS Nd. Moh’d Zahran akitoa maelezo ya kitaalamu kwa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ardhi (Kulia) na Mgeni rasmi Balozi Antilla wa (Katikati).
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi akiwa katika Mkutano na Vyombo vya Habari mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi huo.
…………………………………………………………………………….
(Picha na Miza Othman Maelezo-Zanzibar)
Balozi wa Finland nchini Tanzania
Bi Sinnika Antilla amesema Zanzibar itaondokana na umasikini pindi
itakua na utekelezaji juu ya Sera ya Utunzaji na Utumiaji mzuri wa
Ardhi.
Hayo ameyaeleza katika ukumbi wa Idara ya Ardhi iliyoko
Forodhani Mjini Zanzibar wakati wa Uzinduzi wa Mfumo wa Mtandao wa
Upatikanaji Taarifa za Ardhi Zanzibar unaojulikana kama (Zanzibar Land
Information Service) (ZALIS).
Amesema huo utakuwa na lengo la kushughulikia changamoto za
Ardhi na kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa kuweka sera nzuri za
mazingira nchini Zanzibar.
Aidha amefahamisha kuwa ZALIS ina lengo la kuhakikisha kuwa
Ardhi inatumika vizuri pamoja na kuwepo uongozi ulio bora wa Ardhi
nchini Zanzibar ili ije iwe ni urithi mzuri na wenye manufaa kwa vizazi
vijavyo.
Balozi Antilla ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa
kuanzisha Mtandao wa Serikali (E-Government) uliorahisisha kufanikiwa
kwa mradi huo pamoja na kuushukuru uongozi wa Idara ya Ardhi kwa
ushirikiano wao katika kufanikisha mradi huo wenye malengo makubwa ya
kijamii na kiuchumi kwa nchi hizo mbili.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati
Zanzibar Nd. Ali Khalid Mirza amesema mradi wa ZALIS umepelekea kuwepo
kwa matumizi mazuri ya maliasili hususan Ardhi na Misitu ambapo hadi
sasa zaidi ya 40% ya Ardhi ya Zanzibar imefanyiwa usajili na asilimia
zaidi ya 30% ya Ardhi hiyo inatumika kwa ajili ya kilimo jambo ambalo
limeimarisha kilimo na kupelekea kukua kwa kiasi kikubwa uchumi wa
wananchi wa Zanzibar.
Amefahamisha kuwa mradi wa mtandao huo utasaidia kutunza
kumbukumbu kwa njia iliyo salama ya mtandao na kuepusha kupotea kwa
taarifa za wateja pamoja na kuwataka watendaji wa Idara hiyo kuwapa
elimu wananchi wasio na uelewa juu ya matumizi na umuhimu wa mtandao
huo.
Ametanabahisha kuwa kuna changamoto nyingi zinazoikabili idara
hiyo wakati wa usajili ikiwemo baadhi ya wananchi kutokuwa na vyeti vya
kuzaliwa pamoja na baadhi ya Ardhi kuwa na migogoro ya mirathi hivyo
kushindwa kuzifanyia usajili kwa wakati.
Amesema usajili wa Ardhi ulianza mnamo mwaka 2013 ukianzia na
Mji Mkongwe, Mikoroshoni, Miembeni na maeneo mengine mbalimbali Unguja
na Pemba na hadi sasa bado unaendelea hivyo amewataka wananchi
kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ili kuzifanya Ardhi zao kuwa
katika hali ya usalama kutokana na Dhulma na Wizi jambo ambalo kwa sasa
limekithiri kwa kiasi kikubwa nchini.
No comments:
Post a Comment