Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa
ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akifunga rasmi mafunzo ya siku 14 ya
wasimamizi na wadadisi wa Sensa ya viwanda 2013 itakayofanyika nchini
nzima kuanzia Februari 23,2015. Hafla ya kufunga mafunzo hayo ilifanyika
jana eneo la Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika jijini Dar es
salaam.
Makamu Mkuu wa chuo cha Takwimu
Mashariki mwa Afrika Dkt. Tumaini Katunzi akizungumza na wasimamizi na
wadadisi wa Sensa ya Viwanda itakayofanyika nchi nzima kuanzia Februari
23 mwaka huu jana jijini Dar es salaam wakati wa kufunga mafunzo ya
wadadisi hao.
Baadhi ya wadadisi wa Sensa ya
Viwanda wakifuatilia hafla ya ufungaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa
kukusanya takwimu za Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 iliyofanyika jana
katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika eneo la Changanyikeni
jijini Dar es salaam.
Kamishna wa Viapo ambaye pia ni
Mwanasheria wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Oscar Mangula akitoa ufafanuzi
kwa wasimamizi na wadadisi wa Sensa ya Viwanda (hawapo pichani) kuhusu
Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013
inayotarajia kufanyika nchi nzima kuanzia Februari 23, 2015.
Baadhi ya wadadisi wa Sensa ya
Viwanda wakisaini fomu za viapo vyao mbele ya Kamishna wa Viapo Bw.
Oscar Mangula (hayupo pichani) jana jijini Dar es salaam mara baada ya
kuhitimu mafunzo ukusanyaji wa takwimu za Sensa ya Viwanda 2013
itakayofanyika Februari 23 mwaka huu.
Wadadisi wa Sensa ya Viwanda 2013
wakiapa mbele ya Kamishna wa Viapo Bw. Oscar Mangula (hayupo pichani)
jana jijini Dar es salaam mara baada ya kuhitimu mafunzo ya siku 14 ya
kuwajengea uwezo wa ukusanyaji wa takwimu za Sensa ya Viwanda 2013
itakayofanyika nchi nzima kuanzia Februari 23 mwaka huu.
……………………………………………………………………….
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
SERIKALI imesema kuwa maandalizi
ya Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 itakayofanyika nchi nzima kuanzia
Februari 23 mwaka huu yamekamilika na kuwataka wamiliki wa viwanda na
wadau mbalimbali kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaopita katika
maeneo yao kukusanya takwimu wakati wa Sensa hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya
kufunga mafunzo na kuwaapisha wasimamizi na wadadisi wa Sensa ya Viwanda
ya mwaka 2013 iliyofanyika katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika
jana jijini Dar es salaam , Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa maandalizi ya awali ya Sensa hiyo
yamekamilika yakihusisha uhamasishaji wa ushiriki wa wenye viwanda
kwenye Sensa hiyo, utoaji wa elimu kwa wadadisi na wasimamizi
watakaoendesha zoezi hilo.
Alisema kuwa kutokana na umuhimu
wa Sensa hiyo wamiliki wa viwanda katika maeneo mbalimbali watashiriki
kutoa takwimu zitakazojazwa katika madodoso maalum yaliyoandaliwa ili
kuliwezesha taifa kuweka Sera na mipango ya maendeleo inayotokana na
takwimu sahihi za viwanda vilivyopo nchini
Aliongeza kuwa mafanikio ya Sensa
hiyo yatatokana na wamiliki wa viwanda kutambua na kuithamini Sensa
hiyo kwa kutoa ushirikiano wa kuwapatia takwimu sahihi wadadisi
watakaopita katika maeneo yao kukusanya taarifa zinazohusu masuala
mbalimbali yakiwemo ya uzalishaji wa bidhaa na masuala ya ajira;
Dkt. Chuwa alibainisha kuwa
upatikanaji wa takwimu sahihi kuhusu Sekta ya Viwanda nchini Tanzania
utaiwezesha Serikali kutambua mchango wa viwanda katika ajira,
uzalishaji na pato la taifa hivyo kuweka Sera na mipango endelevu ya
maendeleo itakayoliwezesha taifa na sekta hiyo kupiga hatua
kimaendeleo.
“Sensa hii ya viwanda ni muhimu
kwa maendeleo ya nchi yetu, na mafanikio yake yatatokana na wenye
viwanda kutupa ushirikiano maana bila wao kutoa takwimu sahihi mipango
ya maendeleo kuhusu viwanda haitatekelezeka kwa sababu ya kukosa takwimu
sahihi” Amesisitiza Dkt. Chuwa.
Kuhusu wasimamizi na wadadisi watakaoendesha zoezi hilo
litakalofanyika kwa muda wa miezi 3, Dkt. Chuwa aliwataka wafuate
sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa ili kuwezesha upatikanaji wa
takwimu bora.
Naye Mkurugenzi wa shughuli za
Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Aldegunda Komba akizungumza na
wadadisi hao alisema kuwa wadadisi hao wamepewa dhamana kubwa ya
kutimiza lengo liliowekwa na Serikali la kuwa na takwimu sahihi kuhusu
mchango wa viwanda katika maendeleo ya taifa.
“Mafunzo tuliyowapatia kwa
vitendo na nadharia yamewajengea uwezo wa kukusanya takwimu bora,
tunaomba zoezi hili mlifanye vizuri tunatarajia mtaitumia vizuri elimu
mliyoipata kwa kufanya kazi kwa umakini mkubwa kwa manufaa ya taifa
letu”. Amesisitiza Bi. Komba.
Aidha, alibainisha kuwa kukamilika
kwa Sensa hiyo kutaliwezesha taifa kutambaua mchango wa Sekta ya
Viwanda katika uchumi na pato la taifa.
Kwa upande wake Kamishna wa Viapo
ambaye pia ni Mwanasheria wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Oscar Mangula
akizungumza na wasimamizi na wadadisi wa Sensa hiyo aliwataka
kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia zoezi.
Alisema kuwa zoezi hilo litapata
mafanikio makubwa kufuatia wadadisi na wasimamizi hao kuzingatia mafunzo
na taratibu walizoelezwa huku akibainisha kuwa sheria itachukua mkondo
wake kwa wote watakaoshiriki kwa namna yoyote ile kuvuruga zoezi hilo.
“Napenda niwaeleze kwamba zoezi
hili ni muhimu sana kwa uchumi wa taifa,nawaomba mzingatie yote
mliyoambiwa mtakapokuwa mnakusanya takwimu, zingatieni uadilifu na
utunzaji wa takwimu mtakazopata kwa kuhakikisha mnaziwasilisha kwa
wahusika kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo” Alisisitiza.
No comments:
Post a Comment