Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
Katika maisha ya kila siku, mwananchi anapaswa kutambua wajibu wake katika jamii ikiwa ni pamoja na kutii Sheria bila shuruti. 
Katika
 maisha ya sasa nchini kumekuwa na vitendo vya ukiukwaji wa Sheria 
katika jamii na jamii imekuwa ikihusika katika matendo makubwa ya 
kijinai ambayo ni kinyume na sheria.
Hali hii imekuwa ikitokana na aidha jamii kutojua sheria, na muda mwingine ni kupuuzia tu maagizo na sheria mbalimbali.
Siku
 za hivi karibuni kumekuwepo na ukatili mkubwa ukitendeka katika jamii 
kwa kutokea kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambapo wasiojua 
nini maana ya utu kwa makusudi wanakatiza uhai wa maisha ya binadamu 
wenzao na wengine kuwakata baadhi ya viungo vyao kwa tamaa ya kujipatia 
fedha pamoja na imani za kishirikina.
Jamii
 sio tu inaelewa kuwa kumdhuru mtu ni kosa la jinai bali pia jamii 
inatambua kuwa kuua pia ni kosa kubwa la jinai ambapo katika Sheria ya 
Kanuni ya adhabu Sura ya 16 kifungu cha 197 kimeeleza jinsi ambavyo kosa
 la kuua kwa kukusudia linamgharimu mtu adhabu ya kifo, lakini licha 
kuwepo kwa sheria hiyo, bado jamii inajihusisha na makosa ya kuua kila 
kukicha.
Katika
 mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria, suala la mauaji ya watu wenye Ulemavu 
wa Albino limekuwa ni tatizo kubwa kwani mauaji haya yanafanyika katika 
mazingira tu ya watu kuwa na imani potofu za kuukwaa utajiri wa haraka 
haraka. 
Wakili wa kujitegemea Bwana
 Edwin Webiro anaeleza kuwa watu wengi wanafahamu kuwa kuua ni kosa 
kubwa lenye adhabu ya kifo ama kifungo cha maisha, bado watu hao 
hawajali juu ya uwepo wa Sheria ya kunyonga kwasababu wamekuwa wakiiona 
haitekelezwi ipasavyo, jambo linalowafanya wao waone ni haki kwao 
kufanya unyama wowote kwa watu wasio na hatia (watu wenye ulemavu).
Katika
 hali nyingine jamii pia imekuwa ikikiuka Sheria na kusababisha madhara 
makubwa pale ambapo ajari nyingi zimekuwa zikitokea mfululizo hivi 
karibuni na kusababisha vifo na kuacha ulemavu wa kudumu wa jamii. 
Ajali
 hizi zimekuwa zikisababishwa na uzembe wa baadhi ya madereva wa mabasi 
pamoja na magari madogo kwani kumekuwa na ukiukwaji wa Sheria za 
barabarani ambapo kwa makusudi madereva hao wamekuwa wakikiuka sheria 
mbalimbali na kufanya mambo yanayosabisha ajari. 

No comments:
Post a Comment