MCHAKATO WA BUNGE LA KATIBA NI HALALI – WAZIRI MKUU 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema 
mchakato wa Bunge la Katiba unaoendelea hivi sasa ni halali na kwamba 
mchakato huo ni wa kisheria.
Ametoa kauli hiyo leo mchana 
(Jumapili, Septemba 21, 2014) wakati akizungumza na mamia ya waumini na 
viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa dayosisi mpya ya 
Ziwa Tanganyika ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na 
kuwekwa wakfu Askofu Ambele Anyigulile Mwaipopo aliyeteuliwa kuongoza 
dayosisi hiyo. Dayosisi hiyo inakuwa ya 24 kwa kanisa hilo.
 Waziri Mkuu alikuwa akitoa 
ufafanuzi wa hoja ya Askofu Mwaipopo aliyetaka maoni ya Tume ya 
Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe na Bunge Maalum la Katiba lisitishwe 
kama ambavyo Jukwaa la Katiba limetaka na tamko la Jumuiya za Kikristo 
Tanzania (CCT) limetamka.
Waziri Mkuu alisema: “Rasimu ya 
Katiba iliyowasilishwa na Tume hiyo siyo Katiba bali mawazo 
yaliyokusanywa ambayo yanapaswa kupitiwa na chombo kingine cha kisheria 
ambacho ni Bunge Maalum la Katiba. Mchakato huu halali na mchakato huo 
ni wa kisheria.”
 Alisema muda ambao Tume hiyo 
ilipewa haukuwa mrefu sana kwa hiyo isingekuwa rahisi kwao kuzingatia 
kila eneo linalogusa maisha ya Watanzania. “Mfano suala la ardhi 
halikuelezwa vizuri katika rasimu lakini kwa sasa limeelezwa vizuri 
jinsi ardhi inavyoweza kumnufaisha Mtanzania kwenye kilimo, ufugaji, 
uvuvi na rasilmali misitu,” alisema.
 Alisema kinachowachanganya 
Watanzania ni suala la Serikali mbili au tatu lakini katika makabrasha 
ya Tume ambayo wajumbe wote walipewa, suala la Muungano halikupewa 
kipaumbele na Watanzania wengi waliotoa maoni yao. “Kulikuwa na masuala 
makubwa sita. Suala la ukiukwaji wa haki za binadamu ndilo lilikuwa 
namba moja, suala lililopewa umuhimu wa pili lilikuwa ni la matatizo ya 
huduma za jamii na hilo la muungano lilichangiwa na kundi dogo sana,” 
alisema.
 Alisema kwa mujibu wa takwimu za 
Tume ya Jaji Warioba watu waliotaka Muungano wa Serikali tatu ni kati ya
 asilimia 12 na 13. “Haiwezekani kwa takwimu zile za asilimia 12 hadi 13
 za kutaka Serikali tatu, iamuliwe jumla kwamba ni kwa niaba ya 
Watanzania wengi.”Ili kukidhi shauku ya wengi, Waziri Mkuu alisema yuko 
radhi ifanyike kura mahsusi ya kuwaomba Watanzania waseme kama wanataka 
Muungano na tena uwe ni wa aina gani.
 “Baba Askofu amesema tusitishe 
Bunge la Katiba, hivi sababu hasa ya kusitisha ni nini? Je sote tunajua 
hoja iliyowafanya wenzetu watoke nje na kususia ni ipi? Katika muda wa 
kuchangia kulikuwa na dakika 40 za wengi, dakika 20 za wachache na 
wakapewa dakika nyingine 30 za kuchangia. Muda ule ni mwingi mno kama 
hujaweka mchango wako kwenye maandishi. Badala yake, sote tulishuhudia 
kukashifiana, kejeli na kukashifiana.”
 Aliwasihi Maaskofu, wachungaji na
 viongozi wengine wa dini waliohudhuria uzinduzi huo waendelee kuumboe 
mchakato huo ili uishe vizuri.  
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu 
alimuomba Askofu huyo mpya apokee jukumu hilo kwa mikono miwili na 
kumuahidi kuwa Serikali itasaidiana naye kuwaongoza Watanzania walioko 
kwenye dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha mikoa ya Rukwa na 
Katavi eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 75,140. Kati ya hizo
 km. za mraba 27,713 ni za mkoa wa Rukwa na km. za mraba 47,527 ni za 
mkoa wa Katavi.
Alisema katika dayosisi hiyo mpya 
kuna changamoto nyingi kama vile za malezi ya vijana na watoto, tabia ya
 watu kutopenda kufanya kazi hasa vijana, kukosekana kwa injili kwenye 
maeneo wanayoishi wafugaji na suala la imani za ushirikina.“Asilimia 
kubwa ya Watanzania ni vijana na wao ndiyo Taifa la leo. Ukiangalia 
mavazi ya vijana wa kike (vimini) na wa kiume (mlegezo) hutamani 
kuwaangalia mara ya pili. Msingi mkubwa wa kuwabadilisha hawa wote ni 
malezi ya kiroho. Una changamoto pia ya kufikisha neno la Mungu kwa 
wafugaji ambao ni wengi eneo hili lakini hawana muda wa kuabudu na wengi
 wao hawalijui neno la Mungu, wako bize na mifugo yao.”“Lakini 
changamoto kubwa kuliko zote ni ya kubadili mtazamo wa jamii kuhusu Mkoa
 wa Rukwa hasa kwenye suala la ushirikina. Mtu hata kama hatoki huku 
bado ataweka bango akisema Mganga machachari kutoka Sumbawanga. Baba 
Askofu naomba tushirikiane kupiga sana vita imani hizi potofu kwa sababu
 zinachangia mauaji ya wazee na walemavu wa ngozi,” alisisitiza Waziri 
Mkuu.Mapema, akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kusimikwa rasmi,
 Askofu Mwaipopo aliiomba Serikali isifumbie macho viashiria vyote vya 
upotevu wa amani kwani amani ni tunda la upendo na wala haipatikani kwa 
ncha ya upanga.
 IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
DAR ES SALAAM.
JUMAPILI, SEPTEMBA 21, 2014.

No comments:
Post a Comment