Na: Eleuteri Mangi-Arusha.
Serikali ya Tanzania inaendelea
vema na mpango wake wa kutoa elimu ya msingi kwa watoto wote waliofikia
umri wa kwenda shule nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa wakati akiwasilisha
mada yake inayohusu “Namna Tanzania inavyoboresha Usawa wa Kinga ya
Jamii katika sekta ya elimu” katika kongamano la kimataifa linaloendelea
katika siku ya pili jijini Arusha kuhusu Kinga ya Jamii.
Dkt. Kawambwa alisema kuwa
mpango huo unaanzia elimu ya awali, shule ya msingi na sekondari ambapo
kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule apate elimu ambayo ndiyo msingi
wa kinga ya jamii nchini tofauti na awali ambapo elimu ya msingi ilikuwa
kwa watoto wenye umri kuanzia miaka 7 hadi 14.
Dkt. Kawambwa alisisitiza kuwa
mpango huo wa kinga ya jamii nchini unaenda sanjari na Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) ambao Tanzania imeanza kuutekeleza mwezi Aprili,
2013 ambapo unatarajiwa kuhitimishwa 2017.
Ili kufikia malengo ya kuboresha
mpango wa kinga ya jamii nchini, Dkt. Kawambwa aliwaambia wajumbe wa
kongamano hilo kuwa mbinu zinazotumiwa na Tanzania katika kutekeleza
mpango wa BRN na kuboresha kinga ya jamii ni pamoja na kuboresha vifaa
vya kujifunza na kufundishia shuleni, kusimamamia mpango wa wanafunzi
kujua kusoma, kuandika na kuhesabu na kuboresha ufaulu wa wanafunzi
katika mitihani ya ndani na ya taifa.
Mbinu nyingine ni kuwapa motisha
walimu, kutoa motisha kwa shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya
taifa kwa shule zote iwe ya msingi au sekondari na kuwawezesha walimu na
wanafunzi kujua wajibu wao kwenye sekta ya elimu ili kufikia malengo
yaliyokusudiwa kwa ufanisi ili kuongeza nguvu kazi ya wataalam ambao
ndio msingi wa kuboresha kinga ya jamii na hivyo kupunguza tatizo la
umaskini nchini.
Aidha, Dkt. Kawambwa alisema
kuwa viashiri ambavyo vinaonesha Tanzania inaendelea kupata mafanikio
katika kuimarisha sekta ya elimu na kuimarisha kinga ya jamiina ni
pamoja na kuongezeka ufaulu katika mitihani ya taifa ambapo mwa 2013
ufaulu kwa shule za msingi na sekondari ulikuwa zaidi ya asilimia 60,
mwaka 2014 kwa asilimia zaidi ya 70 na inatarajiwa 2015 ufaulu huo
utaongezeka kufikia asilimia 80.
Akijibu swali la Katibu Mkuu
Wizara ya Kazi, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Huduma Ali N. Ismail
kutoka Kenya aliyetaka kujua kwanini Tanzania bado inatumia mpango wa
kupanga shule katika madaraja ambao unaweza kupunguza morali kwa baadhi
za shule ambazo inaweza kuwa chanzo cha kupunguza uwezekano wa
kutoboresha mpango wa Kinga ya jamii.
Dkt. Kwambwa alisema kuwa
Serikali inasimamia mpango huo kwa kuwahusisha wanafunzi wote na shule
zote bila kubagua na kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, walimu
wamepata mafunzo ambayo yanawawezesha walimu hao kusimamia wanafunzi
wenye mahitaji maalum kulingana na hali zao na amesema Tanzania ipo
tayari kujifunza kutoka Kenya namna wanavyofanikiwa kuacha na mpango wa
kupanga shule katika madaraja.
Kwa upande wa wanafunzi wenye
ulemavu wa ngozi, Waziri Kwawambwa alisema kuwa kwenye suala la mitihani
wanafunzi hao wamepewa kipaumbele kwenye suala la muda ambapo wao
huongezewa baada ya muda wa kawaida wa mtihani kuisha na mitihani yao
imeandikwa kwa maandishi makubwa zaidi ili kuwasaidia kusoma vizuri
zaidi.
Kongamano la kimataifa
linalohusu Kinga ya Jamii linaloendelea jijini Arusha limeandaliwa na
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, Idara ya Kuondo Umaskini
kwa kushirikiana na UNICEF, ILO, UNAIDS na EPRI ambapo washiriki wa
konngamano hilo wanatoka katika nchi za Kenya, Uganda, Bangladesh,
Afghanistan, Msumbiji, Lesotho, Malawi, Afika Kusini, Ghana, Ethiopia,
Zambia, Sudani kusini na mwenyeji Tanzania.
No comments:
Post a Comment