Mshereheshaji mashuhuri nchini Charles Mwakipesile akimfariji mfiwa Nicco Mwaibale mara baada ya kuwasili kijiji cha Newland Kiwira, Tukuyu kwa ajili ya mazishi. |
Nicco Mwaibale akijifuta machozi huku akifarijiwa na kaka yake Kulwa Mwaibale mara baada ya kuwasili kijijini |
Kulwa Mwaibale akimfariji shangazi yake kwa kumfuta machozi mara baada ya kuwasili msibani hapo wakati wa mazishi |
Kulwa (kulia) na Dotto Mwaibale wakati wa mazishi ya mama yao mpendwa |
Vijana wa Skauti wakiusindikiza mwili wa Bibi Twitikege Mlagha katika nyumba yake ya milele. |
Vijana wa Skauti wakiwa wamebeba mwili wa marehemu Twitikege wakiusindikiza kwenye nyumba yake ya milele |
Baadhi ya watoto na wajukuu wa Bibi Twitikege wakilia kwa uchungu wakati wa mazishi yaliyofanyika kijiji cha Newlanda Kiwira. |
Jeneza lenye mwili wa marehemu Twitikege likishushwa kwenye nyumba yake ya milele |
Baadhi ya watoto wa marehemu wakiweka shada la maua kwenye kaburi la mama yao kipenzi |
Umati wa waombolezaji waliohudhuria mazishi ya Bibi Twitikege katika kijiji cha Newland Kiwira Tukuyu wilayani Rungwe. |
Na Rashid Mkwinda
Asubuhi
ya Disemba 13, 1940 huko katika kijiji cha Katumba wilayani Rungwe,
familia ya mzee Mafumu Mlagha ilikuwa katika furaha kwa kumpata mtoto
wa kike baada ya kiu ya muda mrefu ya kuwa na mtoto wa kike.
Ilikuwa ni siku ambayo familia hii ilibahatika kuwa na mtoto wa kike waliyempa jina la Twitikege.
Anga
la kijiji cha Katumba lenye jua lililowakia mandhari nzuri ya kijani
kwenye kijiji kilichoshamiri kilimo cha Migomba na Chai binti wa kike
alizaliwa,Ndege
wa angani na vipepeo wenye rangi nzuri walioruka kutoka mti mmoja
kwenda mti mwingine ilikuwa ni sehemu ya kukamilisha furaha iliyoigubika
familia hiyo na kijiji kwa ujumla.
Twitikege
aliliona jua kwa mara ya kwanza, familia ya Mzee Mafumu Tabulo Mlagha
wa kijiji cha Katumba wilayani Rungwe walijipatia mtoto wa kike
waliyempa jina la Twitikege,walijivunia kuwa na uwiano wa watoto wa
jinsi mbili, kutokana na kuwa na mtoto wa kiume katika zao la kwanza.
Twitikege kama walivyo watoto wengine wa familia ya kabila la Kinyakyusa alikuzwa na kulelewa katika maadili yanayoshabihi mila na desturi za wenyeji wa maeneo hayo.
Aliishi
na kulelewa katika familia ya ukoo wa kichifu, makuzi yake yalikuwa ni
sawa na makuzi ya watoto wengine wa kiafrika waishiyo maeneo ya
vijijini. Katika zama hizo neema ilitawala kutokana na ardhi ya kaya
hizo kustawi kila aina ya chakula na hivyo kumfanya binti Twitikege akue
katika neema.
Maeneo
mengi ya vijijini kwa zama hizo ardhi`ilikuwa na rutubna tele na hivyo
kusheheni mazao ya kila aina na hivyo kufanya uzawa wa wakati huo kuwa
na maisha yenye afya bora kutokana na wingi wa chakula kilichopatikana
katika maeneo hayo.
Kama
ilivyo desturi na mila za kiafrika binti anapofikisha umri wa kuvunja
ungo aliangaliwa na kutunzwa kwa kila hali ambapo Twitikege kulingana na
makuzi ya kimaadili aliyokulia alipofikisha umri wa miaka 13 mwaka 1953
alichumbiwa na kijana wa kijiji jirani na nyumbani kwao cha Mpuga.
Alikuwa ni Anyitike
Gwalamba Mwakwama Mwaibale ambaye kama walivyo vijana wengi wa wakati
huo naye alitokea katika familia iliyostaarabika ya wazazi wachamungu
walioishi kwa maadili kulingana na mila na desturi za maeneo hayo.
Baada
ya kufunga ndoa Twitikege na mumewe Anyitike alichukua dhamana ya
kumlea Twitikege wakaishi vyema nao walirithi desturi njema ya wazazi
wao,waliishi kwa wema na uadilifu na kuahidi kuishi kwa raha mustarehe
katika kipindi chote cha Uhai wao.
Matunda
ya ndoa yao yalibarikiwa na hatimaye wakajaaliwa kupata watoto wake kwa
waume ambao nao waliwalea na kuwasomesha kama walivyolelewa wao enzi za
ujana wao.
Kwa takribani miaka 50 ya ndoa yao walifanikiwa kupata watoto 9 wa kike na kiume,watatu kati yao walitangulia mbele ya haki na kubaki watoto sita.
Kama ilivyokuwa katika malezi yao katika familia zao Twitikege na Mwakwama waliwalea watoto wao kwa maadili na miongozo ya dini bila kusahau mila na desturi za Kinyakyusa ambazo ziliwafanya wamudu kuishi na watu tofauti na kabila tofauti.
Mwaka 2007 ni siku ambayo Bimkubwa huyo Twitikege Mlagha akiwa ametimiza jumla ya miaka 53 ya ndoa yake na mumewe alipata pigo ambalo kamwe hakuweza kulisahau katika maisha yake.
Alimpoteza
mumewe Mzee Anyitike Mwakwama Mwaibale ambaye alifariki na kumuachia
ukiwa, ingawa alipata faraja kwa uwepo wa wajukuu na vitukuu lukuki
waliotokana na watoto wake yeye na mumewe bali pengo la kumpoteza mumewe kamwe halikuweza kuzibwa.
Halikuzibwa
pengo la mumewe ndani ya moyo wake, majonzi na fikra za kumpoteza
mwenzi wake vilitawala katika fikra zake ingawa alipata faraja ya
kutembelewa na wanawe waliokuwa wakiishi maeneo ya mbali na kijijini
kwake.
Mara
kadhaa niliwasikia wanawe wakihitaji kuomba ruhusa katika kazi zao ya
kuja kumuona mama yao na kumpa faraja, ilikuwa ni katika jitihada za
kumsahaulisha machungu aliyokuwa nayo ya kumpoteza mwenza wake aliyeishi
naye tangu akiwa kijana hadi anazeeka.
Alimkumbuka
Anyitike, alikumbuka walivyokuwa vijana, alikumbuka siku ya kwanza
kuchumbiwa na Anyitike, alikosa raha akajikuta akilia peke yake na
kuongezeka majonzi ya kumkosa mumewe ambaye kadri walivyoishi walizoeana
na hata kufikia hatua ya kuwa kama ndugu waliotokana na baba na mama
mmoja.
Ni
takribani miaka saba tangu aondoke mumewe Anyitike, Twitikege kwa
kipindi cha miaka miwili alianza kukumbwa na maradhi ya Uzee na hivyo
kushindwa kujihudumia kwa shughuli alizozoea kujihudumia mwenyewe na
kujikuta akilazimika kuomba msaada kutoka kwa wajukuu na wanawe walio
karibu.
Bimkubwa
huyo aliendelea kuugua na kupata matibabu katika hospitali mbalimbali
za ndani na nje ya mkoa wa Mbeya na hatimaye mwaka 2014 alichukuliwa na
wanawe kuelekea Jijini Dar es salaam kwa ajili ya matibabu.
Ijapokuwa
alikuwa katika maradhi bali aliendelea kuwa faraja kwa wanawe kila
walipomuona wakiwa pamoja wakizungumza naye hili na lile.
Kila
mtoto alipenda kuwa karibu na mama yao ili apate baraka zake hata hivyo
kutokana na maradhi aliyokuwa nayo hakumudu kukaa kwa watoto wote kwa
wakati wote bali alianza kuzidiwa na homa na kulazimika kulazwa
hospitali kwa ajili ya matibabu.
Kila
nyumba ya wanaye alipoenda kuishi nyumba hiyo iligubikwa na furaha na
Baraka,wajukuu na watoto wakitamani kuwa naye wakati wote wakifurahia
uwepo wake katika familia hizo.
Kulazwa
kwake kuliacha simanzi kwa wajukuu na watoto wakikumbuka ucheshi wake
na matarajio yao ya kumuombea walau arejee katikasiha njema ili arejeshe
furaha na Baraka katika nyumba zao kama ilivyokuwa awali.
Haikuwa
bahati tena kwa vitukuu, wajukuu na watoto kumuona Bimkubwa huyu akiwa
katika hali yake ya awali,Mwenyezi Mungu aliamua kumuita.
Kama
ilivyokuwa wakati wa kuzaliwa kwake,tarehe ileile aliyozaliwa ya
Disemba 13 ndiyo hiyo hiyo Disemba 13, 2014 akiwa na jumla ya miaka 74
aliaga dunia usiku wa saa 5:00 Jijini Dar es salaam akiacha majonzi
makuu na vilio kwa vitukuu, wajukuu na wanawe sita waliopo.
Marehemu aliagwa Jijini Dar es salaam na mwili wake kusafirishwa
Mkoani Mbeya katika kijiji cha Newland kilichopo kata ya Kiwira wilayani Rungwe na kuzikwa Disemba 17,2014 katika makaburi yaliyopo katika mashamba ya familia mkabala na kaburi la mumewe kipenzi.
Apumzike kwa amani!!Aamen!!
No comments:
Post a Comment