PICHA NA SAIDI MKABAKULI
………………………………………………………………………………………………..
Na Saidi Mkabakuli, Kagera
Mkoa wa Kagera na maeneo ya jirani
wataanza kujivunia uwanja wa ndege wa kisasa kufuatia kukamilika kwa
Kiwanja cha Ndege cha Bukoba.
Akizungumza na Wakaguzi wa Miradi
ya Maendeleo toka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Meneja Mradi wa
Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kagera, Mhandisi Suleiman Athuman,
amesema kwamba maendeleo ya ujenzi wa jengo la abiria la kiwanja hicho
upo kwenye hali nzuri na mkandarasi atabidhi kazi hiyo mapema mwakani.
“Katika mwaka wa fedha wa 2013/14
kazi zilizopangwa ni ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya kiwanja,
ikijumuisha barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege,
barabara ya kiungio, kwa sasa ujenzi unaendelea vizuri na Mkandarasi
atatukabidhi kazi mapema mwakani,” alisema Mhandisi Athuman.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya
ujenzi wa Kiwanja cha Bukoba, Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa kiwanja
hiko, Mhandisi Pius Gobolo amesema kuwa kazi za usimikaji wa mfumo wa
taa za kuongozea ndege, ujenzi wa jengo jipya la abiria na uzio wa
usalama zimeshakamilika kwa asilimia 80.
“Kama unavyojionea, sehemu kubwa
ya kazi imekamilika, kwa makadirio ni zaidi ya asilimia 80 ya ujenzi wa
kiwanja hiki imeshakamilika,” aliongeza Mhandisi Gobolo.
Kwa mujibu wa mpangokazi wa ujenzi
wa kiwanja hicho hadi kufikia mwezi Juni 2014, hatua iliyofikiwa ni
pamoja na kukamilika kwa ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege,
barabara ya kiungio na maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami; na
ujenzi wa jingo jipya la abiria kufikia hatua ya usimikaji wa paa na
mifumo ya maji safi, maji taka na umeme; na kuendelea kwa ujenzi wa
jengo la abiria na kituo cha umeme.
Naye, Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi
wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi
Florence Mwanri amesema kuwa Serikali imeazimia kuendelea kuboresha
miundombinu ya viwanja vya ndege hususan miradi iliyoibuliwa katika
Programu ya Matokeo Makubwa Sasa.
“Kwa mujibu Programu ya Matokeo
Makubwa Sasa, serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini ipo
kwenye mkakati wa kuuendeleza viwanja vya ndege vyote ili viwe na
kiwango kizuri kwa watumiaji wa viwanja hivyo,” alisema Bibi Mwanri.
No comments:
Post a Comment